CRDB YAZINDUA MSIMU WA PILI WA GRADUATE TRAINESS KUANDAA VIJANA VIONGOZI
DAR ES SALAAM
Katika juhudi za kukuza vipaji vya vijana na kuandaa viongozi wa baadaye katika sekta ya fedha, Benki ya CRDB imezindua rasmi msimu wa pili wa programu ya Graduate Trainees, hatua inayolenga kuwawezesha vijana wenye uwezo kuingia na kung’ara katika soko la ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Mussa Nsekela, alisema kuwa CRDB inaendelea kuwekeza kwa vijana wenye uwezo, ubunifu na maono mapana ili kuimarisha uongozi wa sasa na wa siku zijazo.
Amefafanua kuwa programu hiyo ya miaka mitatu inalenga kutafuta na kukuza vipaji kutoka ndani na nje ya nchi, ikiwahusisha vijana kutoka Tanzania pamoja na mataifa ambayo benki hiyo inafanya shughuli zake, ikiwemo Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na maeneo mengine kama Dubai.
Kwa mujibu wa Nsekela, zaidi ya maombi 4,800 yalipokelewa mwaka huu, lakini baada ya mchakato mkali wa ushindani, vijana 26 pekee ndio waliofanikiwa kuchaguliwa kuanza rasmi programu hiyo.
Amebainisha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na washiriki 18, huku Burundi na DRC zikiwa na washiriki wanne kila moja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utumishi wa benki hiyo, Godfrey Rutasingwa, amesema msimu huu umewaleta pamoja vijana kutoka nchi tatu—Tanzania, Burundi na DRC—ambao tayari wameanza safari ya kukuza uwezo wao kitaaluma na kiutendaji ndani ya benki hiyo.
Ameongeza kuwa huu ni msimu wa pili wa programu hiyo kufuatia mafanikio ya msimu uliopita ulioshirikisha vijana 30 kutoka nchi hizo, ambao walitoa mchango mkubwa katika kukuza biashara ya benki, hasa kupitia ubunifu katika teknolojia na mifumo ya kidijitali.
Naye mmoja wa washiriki wa programu hiyo, Frank Mukwabe, alisema programu hiyo ni fursa muhimu kwa wahitimu wapya wa vyuo vikuu wanaokosa uzoefu wa kazi wanapoingia kwenye soko la ajira.
“Tunatarajia kupitia programu hii kuzalisha viongozi wa baadaye watakaoleta mageuzi katika sekta ya fedha kupitia teknolojia na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania,” amesema.



Comments
Post a Comment