MKUTANO WA KIMATAIFA WA WATAALAMU WA AFYA MOYO KUFANYIKA DAR ES SALAAM, 4 HADI 6
Na Brigiter
DAR ES SALAAM – Mkutano wa Kimataifa wa Wataalamu wa Afya ya Moyo unaojulikana kama Heart Team Africa CardioTan Imaging 2026 International Scientific Conference unatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 4 hadi 6, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Blue Sapphire Hall, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk. Peter Kisenge, amesema mkutano huo utawakutanisha wataalamu wa afya ya moyo kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili maendeleo ya matibabu ya magonjwa ya moyo, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pamoja na kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye changamoto za moyo.
Amesema mkutano huo una manufaa makubwa kwa sekta ya afya na Watanzania kwa ujumla, kwani pamoja na kuimarisha huduma za matibabu, pia utatoa fursa ya kutangaza utalii wa tiba na uwekezaji uliofanyika katika sekta ya afya nchini.
“Mkutano huu utachangia kukuza ubora wa huduma za afya ya moyo nchini na wakati huo huo kuleta fursa za kiuchumi kupitia utalii wa tiba na uwekezaji katika sekta ya afya,”
“Tunatarajia mkutano huu kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa na teknolojia mpya za matibabu ya moyo, huku ukitangaza mafanikio ya Tanzania katika utoaji wa huduma za afya,” amesema Dk. Kisenge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Dk. Idd Lemah, amewataka wataalamu mbalimbali wa afya kushiriki mkutano huo ili kunufaika na mijadala ya kitaalamu itakayolenga kuboresha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kisayansi ya Mkutano huo, Dk. Tatizo Waane, amesema mkutano huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa mikutano mikubwa zaidi ya afya ya moyo barani Afrika, ukikusanya wataalamu wa afya, watafiti na wadau wa sekta ya afya kutoka mataifa mbalimbali.
"Kupitia mkutano huo, Watanzania watanufaika si tu kwa upande wa afya, bali pia kiuchumi kutokana na ongezeko la wageni na shughuli mbalimbali zitakazoambatana na mkutano huo." amesema Dk. Waane.




Comments
Post a Comment