TANZANIA (JKCI) MWENYEJI WA MKUTANO MKUBWA WA KIMATAIFA WA AFYA YA MOYO
Tanzania kuwa kitovu cha Mkutano Mkubwa wa Kimataifa wa Afya ya Moyo 2026
Na Brighitte
DAR ES SALAAM
ZAIDI ya watafiti na wadau wa afya kutoka nchi zaidi ya 60 barani Amerika na Asia wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Kimataifa wa Heart Team Africa Cardio Imaging 2026, utakaofanyika kuanzia Juni 4 hadi 6, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge, amesema mkutano huo wa nne utafanyika katika Hoteli ya New Sapphire, Mbezi Beach, na unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya, hususan magonjwa ya moyo.
Dk. Kisenge amesema mkutano huo utatumia mbinu za kisasa za uchunguzi na vipimo vya afya ya moyo, huku ukiwa pia fursa ya kuonesha maandalizi ya Tanzania katika kupokea wageni wa kimataifa, ikiwemo kuelekea mashindano ya AFCON.
“Kupitia mkutano huu tutashirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo za Andalusia, na kuifanya Afrika kuwa kitovu cha maarifa ya afya ya moyo. Huu ni mkutano wa kwanza wa aina yake barani Afrika unaotoa fursa kwa wataalamu chipukizi kujifunza, kujenga mitandao na kufundishana,” amesema Dk. Kisenge.
Ameongeza kuwa wananchi ndio wanufaika wakubwa wa mkutano huo kutokana na kuimarika kwa ujuzi wa wataalamu wa afya, na kutoa wito kwa wadau, wadhamini na wataalamu kujitokeza kushiriki.
Akizungumzia hali ya magonjwa ya moyo nchini, Dk. Kisenge amesema tafiti zinaonesha kuwa kati ya watu elfu 26 waliopimwa, asilimia 9 walibainika kuwa na matatizo ya moyo, huku shinikizo la damu likitajwa kuwa sababu kubwa.
Amesema mtindo mbaya wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara na matumizi ya pombe ni miongoni mwa vichocheo vya magonjwa ya moyo, akisisitiza kuwa kubadili mtindo wa maisha kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto na Mkurugenzi Mkuu wa Tiba Shirikishi, Dkt. Nice Majani, amesema ongezeko la magonjwa ya moyo linaonekana zaidi kwa sasa kutokana na kuimarika kwa uwezo wa ndani wa kuyagundua mapema.
“Kwa sasa kila watoto 100, mmoja anagundulika kuwa na tatizo la moyo. Zaidi ya watoto 1,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na matatizo ya moyo yanayohitaji upasuaji,” amesema Dkt. Majani.
Ameeleza kuwa matatizo ya moyo kwa watoto yanaweza kuwa ya kuzaliwa au kusababishwa na mazingira, akitaja lishe duni kwa mama mjamzito, ukosefu wa folic acid, matumizi ya pombe, sigara na dawa bila ushauri wa kitaalamu kuwa ni miongoni mwa sababu kuu. Aidha, historia ya magonjwa ya moyo katika familia pia huchangia.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mkutano wa Kimataifa wa Moyo, Dkt. Tatizo Wane, amesema mkutano huo utaambatana na mafunzo ya matumizi ya akili mnemba (AI) katika uchunguzi na ugunduzi wa magonjwa ya moyo, huku wataalamu kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo JKCI, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Muhimbili wakishiriki.
Kwa upande wake, Catherine Malika amesema mikutano ya kitaalamu ni fursa muhimu ya kuongeza ujuzi na kuboresha uwezo wa wataalamu, akiwahimiza wataalamu wa afya kujisajili na kushiriki mkutano huo ili kujifunza zaidi kuhusu teknolojia mpya zinazotumika katika sekta ya afya.
Naye Daktari wa Moyo, Engerasia Kifai, amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya unahitaji wataalamu kuendelea kujifunza ili kutumia kikamilifu vifaa vya kisasa vilivyopo.
“Mkutano huu utasaidia kubadilishana uzoefu na kuongeza ujuzi. Ni wakati wa wataalamu wa moyo kuungana, kuanzisha jumuiya imara itakayosaidia kugundua magonjwa kwa haraka na kuokoa maisha,” amesema Dkt. Kifai.






Comments
Post a Comment