TNCC YAZINDUA SERA YA MAZINGIRA, KUCHOCHEA BIASHARA YA UCHUMI WA KIJANI

TNCC Yazindua sera ya mazingira, yachochea biashara endelevu na uchumi wa kijani Dar es Salaam KATIKA kuimarisha ulinzi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya biashara, Chemba ya Taifa ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TNCC) imezindua Sera ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi ya mwaka 2026, inayolenga kuhimiza ufanyaji wa biashara endelevu na chanya nchini. Akizungumza na Habari leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Rais wa TNCC, Vicent Minja, amesema sera hiyo ni nyenzo muhimu itakayozisaidia biashara kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za mazingira, huku zikiendelea kuchangia kukuza uchumi wa taifa.
Amesema kupitia sera hiyo, TNCC inalenga kuweka misingi ya Sustainable Business Practices zitakazohakikisha ukuaji wa uchumi unakwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali. “Sera hii inalenga kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika biashara rafiki kwa mazingira, kupunguza taka na kuchangia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Minja. Sambamba na uzinduzi wa sera hiyo, TNCC ilitambua na kutoa tuzo kwa kampuni zinazotekeleza biashara jumuishi na dhana ya Uchumi Rejeshi (Circular Economy), hatua inayolenga kuthamini mchango wa sekta binafsi katika kulinda mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kijani nchini.
Minja amesema uzalishaji wa taka kuwa malighafi ni njia mojawapo ya kulinda mazingira na kutoa fursa za ajira, hususan kwa vijana, akisisitiza kuwa taka zinaweza kubadilishwa kuwa rasilimali muhimu endapo zitasimamiwa ipasavyo. Kwa upande wake, mwanzilishi wa kampuni ya Lima Africa, Cathelin Fidolin, ambaye ni miongoni mwa washindi amesema kampuni hiyo inafanya kazi na wakulima katika maeneo ya Geita, Pemba, Mwanza na Tanga, kwa kushirikiana na wanawake na vijana katika ukusanyaji wa taka za kilimo na kuzibadilisha kuwa malighafi. Naye moja ya vijana walioshinda katika utunzaji mazingira kwa matumizi ya taka Taliq Mangachi wa Primo Maggoto Farm Products, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, amesema wanatumia taka mbalimbali kuzalisha bidhaa rafiki kwa mazingira, hatua inayosaidia kutunza mazingira na kutoa ajira kwa vijana. Kwa upande wake, miongoni mwa washindi Mariamu Shardack kutoka taasisi ya Nipe Fagio, amesema taasisi hiyo inatekeleza dhana ya taka sifuri katika eneo la Bonyokwa, Ubungo, kwa kuzalisha mbolea kutokana na taka za matunda na maganda ya mihogo. Amesema mradi huo umefanikiwa kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 30, huku ukiendelea kuchangia katika usafi wa mazingira na uzalishaji wa mbolea asilia. Katika hafla hiyo, washindi wa tatu wa tuzo za biashara jumuishi walipewa zawadi ya shilingi milioni moja kila mmoja, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha na kuwahamasisha vijana kujiajiri kupitia miradi ya uhifadhi wa mazingira na urejelezaji wa taka.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA