WAZIRI JUDITH KAPINGA ATEMBELEA KIWANDA CHA KAMAL GROUP
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ametembelea kiwanda cha Kamal Group kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji zinazoendelea pamoja na kusikiliza changamoto zinazokikabili kiwanda hicho.
Katika ziara hiyo, Waziri Kapinga amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuboresha mazingira ya viwanda, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa taifa.
Amesema Serikali imepokea changamoto zinazohusu upatikanaji wa umeme na maji ambazo zimekuwa zikikwamisha utekelezaji wa shughuli za uzalishaji kwa ufanisi.
Waziri Kapinga ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kupitia taasisi husika, hususa TANESCO na DAWASA, ili kuhakikisha miundombinu rafiki inawekwa kuwezesha viwanda kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Waziri Kapinga amepongeza kiwanda cha Kamal kwa mchango wake katika kukuza ujuzi kwa vijana kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali za mafunzo, hatua inayosaidia kuwaandaa vijana kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kamal Group, Sameer Santosh, amemshukuru Waziri kwa kutenga muda wa kutembelea kiwanda hicho na kuisikiliza changamoto wanazokabiliana nazo.
Amesema kampuni ina matumaini kuwa changamoto za umeme na maji zitapatiwa ufumbuzi ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa zikiwemo gesi na nondo zinazotumika katika ujenzi na shughuli mbalimbali za kijamii.
Naye Ema Mwenda, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kamal Group, amesema kampuni hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake ya uwajibikaji kwa jamii kwa kushirikiana na jamii katika miradi mbalimbali ikiwemo utoaji wa chakula kwa wanafunzi mashuleni na utoaji wa miguu bandia bure kwa watu wenye uhitaji pamoja na kushiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, hususa katika nyumba za maaskari Kigamboni na mashuleni.
Aidha, Mwenda ameeleza kuwa Kamal Group inaendelea kupanua shughuli zake katika eneo la Kerege, Mkoa wa Pwani, ambako kuna miundombinu yote muhimu ya viwanda, na kutoa wito kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika eneo hilo.
Ziara hiyo imelenga kupata uelewa wa kina kuhusu michakato ya uzalishaji, uwezo wa kiutendaji wa kiwanda, pamoja na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.
Maafisa wa wizara waliokuwepo walisema ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Viwanda na Biashara kuimarisha ushirikiano na viwanda vinavyochangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika ziara hiyo, Waziri Kapinga alipatiwa maelezo ya kina kuhusu shughuli za uzalishaji za Kamal Group na kutembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda.
Majadiliano yalijikita katika masuala ya uzingatiaji wa kanuni na miongozo ya sekta ya viwanda, pamoja na nafasi ya sekta ya uzalishaji katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.
Kamal Group ni miongoni mwa makampuni makubwa yanayofanya shughuli zake katika sekta ya viwanda nchini Tanzania, yakichangia katika utoaji wa ajira na ongezeko la uzalishaji wa viwandani.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa mazungumzo kati ya viongozi wa Serikali na menejimenti ya kampuni kuhusu mikakati ya kukuza sekta ya viwanda na ushirikiano wa pamoja kwa maendeleo endelevu.



Comments
Post a Comment