CRDB YATENGA Sh450 MILIONI KUFANIKISHA BUNGE GRAND BONANZA 2026

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imekabidhi vifaa vya michezo na zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa CRDB Bank Bunge Grand Bonanza litakalofanyika Juni 20, 2026 katika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Dodoma, huku Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi. Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo leo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa, amesema benki hiyo imetenga jumla ya Sh450 milioni kufanikisha bonanza hilo ambalo mwaka huu litakuwa na ushiriki wa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania. Amesema ushirikiano wa muda mrefu kati ya Benki ya CRDB na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haujajikita katika utoaji wa huduma za kifedha pekee, bali pia katika kuunga mkono maendeleo ya jamii kupitia shughuli mbalimbali za kijamii. "Ushirikiano wetu hauishii kwenye huduma za fedha pekee bali unaimarishwa zaidi kupitia shughuli za kijamii na maendeleo ya wananchi, ikiwamo utekelezaji wa Programu ya Imbeju inayosimamiwa na CRDB Bank Foundation yenye lengo la kukuza elimu ya fedha, kujenga uchumi jumuishi na kuwawezesha wananchi kupata mitaji," amesema Mwambapa. Katika hafla hiyo, Mwambapa alimkabidhi Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Mbunge Festo Sanga, vifaa mbalimbali vya michezo ikiwamo trakisuti 1,000, fulana 1,000, seti mbili za jezi za mpira wa miguu, seti mbili za mpira wa pete, seti nne za mpira wa kikapu, seti nne za mpira wa wavu, pamoja na kofia 1,000, medali 1,200 na makombe tisa.
Akipokea vifaa hivyo, Sanga amesema bonanza hilo litaanza kwa matembezi ya pamoja kabla ya kuendelea na michezo ya bao na karata, huku jioni timu za wabunge zikitarajiwa kucheza dhidi ya mabalozi katika mpira wa miguu. Aidha, katika mpira wa pete na mpira wa kikapu, wabunge watavaana na wafanyakazi wa Benki ya CRDB. "Mchezo ni afya, hivyo tunawaalika Watanzania wote kujitokeza kushiriki na kuwashabikia wabunge pamoja na viongozi wao, huku wakijifunza umuhimu wa kufanya mazoezi kwa ajili ya afya bora," amesema. Sanga ameishukuru Benki ya CRDB kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha bonanza hilo na kuendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini.
"Ushirikiano huu ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi na taasisi za umma zinavyoweza kushirikiana kuhamasisha michezo, kujenga afya njema na kuimarisha umoja miongoni mwa viongozi na wananchi," amesema. Akizungumzia umuhimu wa diplomasia ya michezo, Sanga amesema uzoefu alioupata aliposhiriki mbio za CRDB Bank Marathon nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeonyesha jinsi michezo inavyoweza kuunganisha watu wa mataifa mbalimbali. "Mbio hizi zimeonyesha nguvu ya diplomasia ya michezo katika kuwaleta pamoja watu wa mataifa tofauti bila kujali hali zao za kiuchumi. Ndiyo maana mwaka huu tumewaalika mabalozi kushiriki Bunge Grand Bonanza ili kupanua ushirikiano na kuimarisha mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine kupitia michezo," amesema.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA