DAR CITY USO KWA USO NA JKT
TIMU ya mpira wa kikapu ya JKT leo Juni 17, 2026 itashuka dimbani kuikabili Dar City katika mchezo wa Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam utakaochezwa kwenye Uwanja wa Don Bosco Oysterbay (Mbuyuni) kuanzia saa 2:00 usiku.
-
JKT wanaingia kwenye pambano hilo wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 11 baada ya kucheza michezo saba. Katika michezo hiyo, wamefanikiwa kushinda minne huku wakipoteza mitatu.
-
Kwa upande wa Dar City, mabingwa hao wa Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam wamecheza michezo mitatu pekee kutokana na kuwa katika majukumu ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Basketball Africa League (BAL) yaliyofanyika nchini Rwanda wakati ligi ikiendelea.
-
Licha ya kucheza michezo michache, Dar City wameanza vizuri kampeni yao ya ligi kwa kushinda michezo yote mitatu waliyoicheza na kujikusanyia alama sita, hali inayowafanya kuwa miongoni mwa timu zinazofuatiliwa kwa karibu katika mbio za ubingwa.
-
Wakati huo huo, mchezo mwingine wa ligi hiyo utawakutanisha Pazi dhidi ya UDSM Outsiders. Mchezo huo utachezwa katika uwanja huo huo wa Don Bosco Oysterbay kuanzia saa 12:00 jioni.
Mashabiki wa mpira wa kikapu wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo hiyo miwili muhimu katika harakati za timu mbalimbali kusaka pointi za kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi.



Comments
Post a Comment