UNDP YAWAZAWADIA WANAFUNZI 20 SH MILIONI 70 STUDENT FOUNDERS FELLOWSHIP
UNDP Tanzania Yawazawadia Wanafunzi Wajasiriamali 20 Zaidi ya Shilingi Milioni 70 Kupitia Awamu ya Pili ya Youth Ignite Student Founders Fellowship
Wanafunzi wajasiriamali ishirini kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini wamepatiwa zawadi za fedha taslimu zaidi ya Shilingi milioni 70 kufuatia shindano la uwasilishaji wa mawazo ya biashara lililoandaliwa chini ya mpango wa Youth Ignite Student Founders Fellowship – Awamu ya Pili.
Mpango huo unatekelezwa kupitia Programu ya FUNGUO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania, kwa ufadhili wa pamoja wa Serikali ya Uingereza kupitia Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Finland.
Shindano hilo liliwakutanisha wanafunzi 30 kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, waliowasilisha mawazo bunifu ya biashara yenye mchango chanya kwa jamii mbele ya jopo la majaji. Tukio hilo limeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ujasiriamali na ubunifu miongoni mwa vijana wa Kitanzania.
Mbali na kupokea zawadi za fedha taslimu, wanafunzi wajasiriamali walipatiwa pia msaada wa kitaalamu, ikiwemo mafunzo ya maendeleo ya biashara, ushauri elekezi (mentorship), pamoja na maandalizi ya kuwafanya wawe tayari kuvutia wawekezaji wapya.
Akizungumza na Habari Leo, Dkt. Harun Makandi, Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alisema mpango huo unaendana kikamilifu na ajenda ya Serikali ya kukuza ubunifu, utafiti wenye tija kibiashara na ujasiriamali miongoni mwa vijana.
“Mpango huu unaunga mkono moja kwa moja jitihada za serikali za kulea kizazi kipya cha wabunifu na wazalishaji wa ajira mpya kinachotoka katika taasisi zetu za elimu ya juu. Unaakisi mwelekeo wa Tanzania wa kuunganisha sayansi, teknolojia na ujasiriamali katika maendeleo ya taifa,” alisema Dkt. Makandi.
Kwa upande wake, John Rutere, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, alisema ushirikiano huo unachangia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya muda mrefu ya maendeleo ya nchi.
“Jukumu la UNDP nchini Tanzania limejikita katika kuunga mkono Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 (DIRA 2050), inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kwa kufikia uchumi wenye thamani ya Dola za Kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Kufikia dira hii kunahitaji uwekezaji wa makusudi kwa vijana na biashara zao,” alisema Rutere.
Aliongeza kuwa programu kama Youth Ignite Student Founders Fellowship ni mifano halisi ya miradi inayowawezesha vijana kwa ujuzi, mitandao ya wawekezaji na mitaji inayohitajika kujenga biashara zenye uwezo wa kukua na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Washirika wa maendeleo walichangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kundi hili la washiriki. Euan Davidson, Kiongozi wa Timu ya Miradi Endelevu kutoka FCDO, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika biashara zinazoongozwa na vijana kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi jumuishi.
Kwa upande wao, Westerwelle Foundation Tanzania na StartHub Africa walitoa mafunzo ya vitendo ya ujasiriamali, ikiwemo maandalizi ya uwasilishaji wa mawazo ya biashara (pitch development), ili kuhakikisha washiriki wanakuwa tayari kuvutia wawekezaji kabla ya mashindano.
Naye Sanna-Liisa Taivalmaa, Mkuu wa Ushirikiano katika Ubalozi wa Finland, alithibitisha dhamira ya Finland kuendelea kuunga mkono mifumo ya ubunifu na ujasiriamali wa vijana kama sehemu ya vipaumbele vya ushirikiano wa maendeleo.
Miongoni mwa washindi waliofanya vizuri zaidi, kila mmoja alipokea Shilingi milioni 6 kwa ajili ya kukuza biashara zao. Mmoja wao ni Herriet Nairumbe, Mwanzilishi wa Niches Food Products yenye makao yake Arusha, inayojihusisha na uongezaji thamani wa mazao ya pilipili na matunda.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Herriet alisema fedha hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji na kupanua masoko.
“Fedha hizi zitatumika kununua mashine itakayorahisisha uzalishaji na kuongeza tija. Pia tunapanga kuwekeza katika masoko ya mikoa mingine ili bidhaa zetu ziwafikie watu wengi zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa kupitia programu hiyo wamejifunza utunzaji wa kumbukumbu za kifedha, upangaji wa bei, ujenzi wa timu na huduma kwa wateja, hatua zinazosaidia biashara yao kukua na kutoa ajira kwa vijana wengine.
Mshindi mwingine ni Irene George Ngatibigwa, Mwanzilishi Mwenza wa Eco Mushroom, kampuni inayojihusisha na uzalishaji wa uyoga mbichi, uliokaushwa, unga wa uyoga na vitafunwa vinavyotokana na uyoga.
Irene alisema changamoto ya awali ilikuwa ni ukosefu wa miundombinu ya kupanua uzalishaji na kufikia masoko makubwa.
“Nilikuwa napata oda lakini sikuweza kuingia mikataba kwa sababu sikuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya usambazaji,” alisema.
Alieleza kuwa Shilingi milioni 6 alizopata zitamsaidia kununua vifaa, kuboresha miundombinu ya uzalishaji na kuajiri vijana zaidi katika uzalishaji na masoko.
Baada ya kushiriki programu hiyo, Irene alisema mtazamo wake wa kibiashara umebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Kabla ya kujiunga na programu hii nilikuwa nafanya biashara kwa mapenzi binafsi bila ujuzi rasmi wa masoko au uwasilishaji kwa wawekezaji. Kupitia mafunzo, nimejifunza masoko, uwasilishaji na kujenga mitandao ya wawekezaji. Ujuzi huu utakuwa muhimu sana tunapopanua biashara yetu,” alisema.
Kwa ujumla, Youth Ignite Student Founders Fellowship inaendelea kujenga kizazi cha biashara za wanafunzi zenye uwezo mkubwa wa kukua, kuunda ajira na kuchangia mabadiliko chanya ya kiuchumi nchini Tanzania. Washindi wanawakilisha sekta mbalimbali ikiwemo teknolojia, kilimo-biashara, suluhisho za mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji viwandani na ubunifu wa kijamii.









Comments
Post a Comment