OVAH YANAPINGA MANENO YA UDHALILISHAJI
Na Brigitte Davis
TAASISI ya Ovah Tanzania imesema inapinga maneno ya udhalilishaji yanayotolewa kwa wanawake kwenye maeneo ya wazi ya kijamii kwa kuwa kuyachukulia kawaida kunamfanya mwanamke ajihisi hayuko salama.
Hayo yamesemwa Dar es Salaam juzi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Modesta Joseph kwenye uzinduzi wa mradi wa Jamii Salama Initiative (JSI) utakaotumika kutoa elimu dhidi ya maneno ya udhalilishaji kwa wanawake, program itakayofanywa kwa ushirikiano na taasisi nyingine mbalimbali.
Modesta alisema baadhi ya maneno wanayoitwa wanawake kwenye maeneo ya Masoko, kwenye vituo vya mabasi a mitaani yakiwemo Chura, Paka na mengine yanayoashiria udhalilishaji yanapaswa kukemewa na kila mmoja kwa usalama wao.
"Ni maneno machafu ambayo yamekuwa yakiwafanya wanawake wengi hawana amani, tumekuja na mradi wa JSI ili tuendelee kutoa elimu kwa madereva, masokoni na maeneo mengine ya wazi umuhimu wa kuheshimiana na kulindana ili kutengeneza jamii salama,"alisema.
Alisema pia, wapo watu wenye tabia ya kubambia wanawake kwenye daladala na wengine mitaani huwashika wanawake kwenye maeneo tofauti ya mwili pasiporidhaa kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia.
Mkuu huyo alisema tayari wametengeneza mabango madogo yenye matangazo na video mbalimbali kuelimisha jamii yapi ni sahihi na yapi sio sahihi na wapi pa kuripoti ikiwa watatendewa ukatili na kuhimiza jamii kuungana nao kuleta mabadiliko chanya.
Program Ofisa wa Ovah Ilham Mohamedalisema wahusika wengi wa ukatili ni wanaume na hivyo, wamekuwa wakiongea nao na wataendelea kuwapa elimu ili wote kwa pamoja waungane kukemea udhalilishaji na ukatili wa kijinsia.
"Wanaume wanatakiwa wawe mfano wa mabadiliko tunayotaka. Tunatamani wajitokeze kutengeneza jamii ambayo ni salama, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha kila mtu anapata haki zake,"alisema.
Naye Kiongozi wa Idara ya Mawasiliano wa Taasisi ya Sesema Faith Mkonyi alisema jamii imekuwa haina uelewa juu ya ukatili wa kingono kwa kufikiri ni tendo tu la ubakaji pekee ndio maana kuna haja ya kutoa elimu zaidi ili watu wasiendelee kufanya makosa.
Alisema changamoto walizoziona jamii imevihalalisha baadhi ya vitu na maneno makali yanayosikika kwa kuona ni kawaida lakini havipaswi kuwa hivyo huku akiomba serikali kuweka miundombinu ya taa za kutosha barabarani kuhakikisha usalama wa Kila mmoja wakati wote.
Mwisho

Comments
Post a Comment