DULLA MBABE KUSAFISHA NGUMI MAUGO
Na Brighitte Davis
BONDIA wa ngumi za kulipwa, Abdallah Pazi 'Dullah Mbabe' amesema anaenda kumstafisha ngumi mpinzani wake, Mada Maugo katika pambano la 'Taji la Mama Samia' litakalofanyika Desemba 26, mwaka huu.
Dullah Mbabe atapanda ulingoni kuzichapa pambano kuu dhidi ya Maugo la raundi nane, uzito wa juu ( kilo 76) litakalofanyika Muleba Mkoani Kagera.
Akizungumza Dar es Salaam leo katika uzinduzi wa pambano hilo, Dullah Mbabe amesema baada ya kukaa kimya muda mrefu bila kupanda ulingoni awamu hii amejipanga kuja kuleta mapinduzi katika ngumi kwa kumchakaza mkongwe huo mwenzake.
"Nimejipanga salama kiafya naendelea vizuri, naenda katika vita dhidi ya Mada Maugo, baada ya kupoteza mapambano machache ikiwemo la Erick Katompa naenda kuonyesha kazi mkoani Kagera,"amesema.
Amewatoa hofu wakazi wa Muleba na kuwataka wakae mkao wa kula wategemee mambo mazuri kutoka kwake kwani siku hiyo atamuonyesha kazi kwa sababu mara ya kwanza alimtengua kiuno awamu hii anaenda kumstafisha.
Mratibu wa matukio kutoka Kampuni ya Peak Time, Bakari Khatibu ambao ndiyo waandaji wa pambano hilo amesema awamu hii wanaenda kuweka historia Muleba kutokana na mapambano yaliyopo kuwakutanisha wababe.
Upande wake Karim Mandonga amesema mpinzani wake, Said Mbelwa hatamaliza raundi ya pili kutokana na maandalizi anayoyafanya.
Amesema anaenda mkoani Kagera kuonyesha ngumi mpya itwayo 'Kiberege' ambayo itaenda kumpiga mpinzani wake, Mbelwa.
Mbali ya mabondia hao mapambano mengine ambayo siku hiyo yataenda kuonyesha kazi ni pamoja na Osama Arabi atacheza na Peter wakati Anuari Mlawa dhidi ya Rashidi Matumla huku Jamali Kunoga atazichapa na Khalidi Kunoga wakati Happy Daudi dhidi ya Hidaya Zahoro.
Mwisho

Comments
Post a Comment