KAMPUNI YA JAN INTERNATIONAL IMETUNZA WATEJA WAKE
Kampuni ya kuuza magari ya Jan international Ltd imewatunza wateja wake wanne gari, pikipiki, jokofu na simu ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuwashukuru kwa kuwaunga mkono.
Washindi hao wametokana na droo waliyoichezesha juzi baada ya kampeni ya kuendesha zoezi hilo iliyofanyika kwa zaidi ya mwezi mmoja kwa kukusanya karasi walizopewa wajaze watu wote waliokwenda kununua magari kwenye kampuni hiyo.
Washindi hao ni Edwin Godwin alishinda gari aina ya Harrier anaconda, Harun Rajabu alishinda pikipiki, Agnes Nganile alishinda jokofu na tv inchi 52 na Issa Tambuu alishinda simu aina ya Iphone 16 pro max.
Mshindi wa gari Godwin alisema ametoka kununua gari mwezi uliopita na wakati anapewa karatasi ajaze hakuamini alikuwa anaona kama anapoteza muda wake akiamini huwa wanachaguliwa na kueleza furaha yake baada ya kuona ni kweli.
"Mwanzoni sikuamini kumbe ni kweli, nashukuru sana Jan kwa kututhamini wateja wao msimu huu wa sikukuu mmetutia moyo na kutuhamasisha kuendelea kuwa wateja wenu,"alisema baada ya kupigwa simu aje kwa kuwa hakuwepo wakati anatangazwa.
Kwa upande wake, Haruni aliyepata pikipiki ya boxer alisema atatumia chombo hicho kama usafiri wake wa kwenda kwenye shughuli zake huku Agnes akisema yeye hakutegemea kushinda anamshukuru Mungu kwa zawadi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Ally Akibar aliwapongeza washindi wote na kusema hicho walichokifanya msimu huu wa sikukuu watakiendeleza na mwakani ambapo wataongeza idadi ya zawadi ya magari ili washindi wawe wengi.
Pia, katika kusherehekea sikukuu za kristmas na mwaka mpya msimu huu wametangaza punguzo la asilimia 50 kwa magari 500 na kuwahimiza wateja wao kutumia muda huu kabla ofa hiyo haijaisha.
Miongoni mwa mashuhuda waliokuwa wakizungusha gurudumu la droo hiyo ni mastaa wa michezo na burudani bondia Mfaume Mfaume aliyesema:" Ni vizuri makampuni kuwathamini wateja wao umeona kuna waliopata gari, pikipiki na zawadi nyingine na hata watu wengine wanaofuatilia au wamepanga kununua gari wakiona Jan international inavyothamini wateja wao inatia moyo,"
Rapa Fareed Kubanda 'Fid Q' alisema ameona wenye bahati zao watakwenda kusherehekea sikukuu wakiwa na furaha na kwamba amejifunza na kuhamasika kuwa akinunua gari pengine hapo ni mahali sahihi kwasababu ataingizwa kwenye droo na kuweza kupata gari na zawadi mbalimbali.
Hamad Seneda 'Madee' alisema amepata funzo kwamba ndoto ambazo wengi wanaotaka sio za uongozi tu lakini ghafla mtu anapigiwa simu anaambiwa aje achukue gari ni jambo linalofurahisha na kuzihimiza kampuni nyingine kuiga kwa ajili ya kuthamini wateja wao.
Mwisho



Comments
Post a Comment