AFRICA KUKUTANA ARUSHA MKUTANO WA TEKNOLOJIA YA AKILI MNEMBA (APAIC 2025) NOVEMBA 24 HADI 27
Washiriki zaidi ya 1,200 kutoka nchi zaidi ya 40 wanatarajiwa kushiriki Mkutano wa Kilele wa Akili Unde Afrika (APAIC 2025) utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Novemba 24 hadi 27, 2025, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kimataifa litakalojadili matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba (Unde) katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, biashara na utawala bora.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa APAIC 2025, Abdulwahid Ali Khamis, alisema tukio hilo litaweka historia mpya katika safari ya mageuzi ya kidijitali barani Afrika, likilenga kuunganisha serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za elimu na wabunifu wa teknolojia.
“Afrika ipo katika kipindi muhimu cha kuamua njia ya mageuzi yake ya kijamii na kiuchumi kupitia akili unde. Huu ni wakati wa kuweka misingi ya matumizi jumuishi, bunifu na yenye maadili ya teknolojia hiyo,” amesema Khamis.
Ameeleza kuwa mkutano wa mwaka huu umejikita katika dhima ya ‘Mapinduzi ya Agentic AI’, teknolojia ya kizazi kipya inayoitwa Agentic Artificial Intelligence, ambayo inauwezo wa kujifunza, kufanya maamuzi na kuchukua hatua kwa ushirikiano na binadamu.
“Hii ni hatua muhimu katika historia ya Afrika. Teknolojia ya Agentic AI inakwenda mbali zaidi ya kuchambua taarifa – sasa inaweza kufanya maamuzi na kushirikiana na binadamu kwa wakati halisi, jambo linaloweza kubadilisha huduma za kijamii na kiuchumi,” amefafanua.
Khamis alibainisha kuwa APAIC 2025 itakuwa jukwaa la kuonesha namna akili unde inavyoweza kuleta mageuzi katika utawala, uchumi, na ubunifu wa kijamii kwa kuzingatia maadili, usalama wa taarifa na faragha za watumiaji.
Katika mkutano huo, viongozi wa teknolojia, watunga sera, wataalamu wa sayansi na wabunifu kutoka ndani na nje ya Afrika watashiriki kujadili ramani ya pamoja ya maendeleo ya akili unde barani Afrika.
Aidha, Khamis amesema mkutano huo utashuhudia utiaji saini wa Azimio la Mombasa kuhusu matumizi salama na yenye maadili ya akili unde, pamoja na uzinduzi wa mpango maalum wa kimataifa uitwao ‘The Dawn Directive’ unaolenga kuweka misingi ya matumizi bora ya Agentic AI.
Kwa mujibu wa Khamis, tukio hilo pia litatoa fursa kwa vijana wabunifu na kampuni changa za teknolojia kuonesha miradi yao ya kiteknolojia, huku washiriki kutoka taasisi za elimu, sayansi na maendeleo wakitarajiwa kuonesha tafiti zao kuhusu matumizi ya akili unde katika ustawi wa jamii.


Comments
Post a Comment