UVCCM YAKEMEA VURUGU ZA OKTOBA, AMANI NI MSINGI WA MAENDELEO

UVCCM Yakemea Vurugu za Oktoba, Yasema Amani ni Msingi wa Maendeleo DAR ES SALAAM:MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) amelaani na kuvunja ukimya, kwa masikitiko makubwa kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29 na 30, 2025, ambayo amesema kwa kiasi kikubwa yalihusisha vijana. Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa (UVCCM) Mohamed Kawaida amesema kuwa matukio hayo yameacha majeraha makubwa katika jamii, hasa ikizingatiwa kuwa yalifanywa na kundi la watu ambalo yeye mwenyewe ana dhamana ya kuwaongoza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). “Leo nimesimama mbele yenu si kwa furaha, bali kwa huzuni kubwa moyoni mwangu. Uchaguzi uliopita ulioleta matokeo mazuri kwa chama chetu, umeambatana na vurugu na fujo ambazo zimeacha alama za maumivu na hasara kubwa kwa taifa,” amesema . Ameongeza kuwa kitendo cha vijana kushiriki katika vitendo vya vurugu ni kinyume cha maadili, sheria na utaratibu wa kijamii, huku akisisitiza kuwa vitendo hivyo vimeathiri ustawi wa taifa.
Aidha, Kawaida ameeleza kuwa baadhi ya watu walioratibu vurugu hizo hawapo nchini, na wengi wao si raia wa Tanzania, bali waliwahamasisha vijana kupitia mitandao ya kijamii kufanya fujo huku wao wakistarehe nje ya nchi. “Wanaichoma moto nchi yetu huku wao wakilipwa pesa na wale waliowatuma. Bahati mbaya vijana wetu waliwarubuniwa, wakidhani ni mkusanyiko halali wa kutoa maoni, kumbe lengo lilikuwa kuleta vurugu,” ameongeza. Kawaida amesisitiza kuwa vurugu hizo hazina tija yoyote kwa taifa, bali zimeleta uharibifu mkubwa wa mali na vifo vya watu wasio na hatia. Ametoa mfano wa baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam ambapo vituo vya mabasi, vituo vya polisi, maduka na vituo vya mafuta viliteketezwa kwa moto. “Vurugu hizi si demokrasia, ni uhalifu. Uhuru wa kuandamana haumaanishi uhuru wa kuharibu mali au kuhatarisha maisha ya wengine,” amesema. Kwa mujibu wake, vurugu hizo zilisababisha hasara kubwa katika sekta ya biashara na uchumi, kwani shughuli nyingi zilisimama, hususan jijini Dar es Salaam, na hivyo kuathiri maisha ya wananchi wengi hasa wenye kipato cha chini. Aidha, ameeleza kuwa athari hizo hazikuishia ndani ya mipaka ya Tanzania pekee, bali pia zimeathiri biashara za kikanda kwa nchi jirani kama Kenya, Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi, Congo na Uganda ambazo hutegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa bidhaa. “Vijana wenzangu, mnapofanya vurugu hapa nyumbani, maumivu yake hayabaki Tanzania pekee — yanawafikia pia vijana wa nchi jirani wanaotegemea amani yetu kwa ustawi wa biashara,” amesema Kawaida. Amesisitiza kuwa amani ni urithi muhimu uliojengwa tangu uhuru wa taifa, na ndio msingi wa maendeleo na uwekezaji nchini. “Amani si udhaifu, bali ni nguvu ya maendeleo. Hebu tushikamane na tuzungumze kwa amani, si kwa vurugu,” amehimiza. Katika kumalizia, Kawaida amewataka vijana, wazazi, viongozi wa dini na wanasiasa kushirikiana katika kuhimiza amani, umoja na mazungumzo yenye tija badala ya maneno ya uchochezi au kejeli. “Natoa rai kwa wanasiasa wote wa chama changu na wasio wa chama kuacha kauli zinazoweza kutugawa au kuleta taharuki. Huu ni wakati wa kujenga, sio kubomoa,” amehitimisha.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA