MWAKINYO KUWANIA HESHIMA YA TAIFA LEO WARE HOUSE

BONDIA wa kimataifa Hassan Mwakinyo leo anaipeperusha bendera ya Tanzania katika pambano kubwa la Boxing on Boxing Day dhidi ya mpinzani wake kutoka Nigeria, Stanley Eribo, litakalofanyika Desemba 26, 2025, katika Ukumbi wa Warehouse, Masaki jijini Dar es Salaam. Mwakinyo, ambaye ameongoza zoezi la upimaji uzito pamoja na mabondia wengine, amesema yuko tayari kikamilifu kwa pambano hilo, akiahidi ushindi kwa Watanzania. Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mwakinyo alisema amejiandaa kwa kiwango cha juu na yuko tayari kumpambana mpinzani wake kwa nguvu zote.
“Nimejiandaa vizuri sana kwa pambano hili. Nimemuandaa mpinzani wangu kikamilifu na nawahakikishia Watanzania ushindi mkubwa. Nitaingia ulingoni kuipigania heshima ya taifa,” amesema Mwakinyo. Kwa upande wake, bondia wa Tanzania Hamadi Furahisha amesema maandalizi yake yamekamilika na yuko tayari kukabiliana na mpinzani wake kutoka Malawi, Hanock Phiri. “Najua ninampinzani mkali, lakini niko tayari kumpa pambano gumu na kuwaburudisha mashabiki,” amesema Furahisha. Naye bondia kutoka Nigeria, Stanley Eribo, amesema amekuja Tanzania kwa lengo la kushinda pambano hilo, Akisisitiza kuwa licha ya heshima iliyopo, ulingoni ni mapambano.“Nimekuja Tanzania kwa ajili ya ushindi. Heshima ipo, lakini ulingoni nitapambana kwa nguvu zangu zote,” amesema Eribo.
Katika upande wa wanawake, bondia Debora Mwenda amesema yuko tayari kuiwakilisha vyema Tanzania katika pambano lake dhidi ya bondia kutoka Malawi, Mariam Dick. “Nimefanya maandalizi ya kutosha. Natambua ukubwa wa pambano, lakini niko tayari kuwakilisha wanawake wa Tanzania kwa ushindi,” amesema Debora. Mratibu wa matukio kutoka kampuni ya Peak Time, Bakari Hatibu, amesema maandalizi ya tukio hilo yamekamilika kwa asilimia 90, huku mabondia wote wakiwa tayari kuingia ulingoni. “Mabondia wote wamewasili salama na maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa. Kilichobaki ni mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani kubwa ya kufunga mwaka,” amesema Hatibu. Katika mapambano mengine ya usiku huo, Ally Ngwando atachuana na Mussa Makuka, huku pambano hilo pamoja na mengine yakitarajiwa kutoa burudani kubwa kwa mashabiki wa mchezo wa ngumi.

Comments