MITIHANI ALIZOPITIA DR TAX



Hii ndiyo mitihani migumu iliyowahi kumkabili Dk TAX

Simulizi ya safari ya elimu na Utumishi wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ni historia inayosisimua, ikihusisha nyakati ngumu na juhudi kama ufunguo wa nyakati hizo.

Pengine kila anayeonekana na mafanikio leo, zipo nyakati ngumu alizopitia jana ambazo kama si kukomaa asingeupata umaarufu alionao.

Katika hili, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ni kielelezo sahihi, anayesimulia magumu aliyowahi kupitia katika safari yake ya kuisaka elimu.

Kwa mujibu wa waziri huyo ambaye ni mwanamke wa kwanza kuiongoza wizara hiyo, magumu hayo yalitokana na kigugumizi cha nini alipaswa kuchagua kati ya kulea mtoto au kwenda nje ya nchi kujiendeleza na elimu.

Ingawa wakati huo, mwanawe huyo alikuwa na umri wa miaka minne, anasema kwa mzazi isingekuwa rahisi kukubali kumwacha kisha asafiri kwenda nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka.

Kudharauliwa kutokana na jinsi yake, maswali yenye chembechembe za ukandamizaji wa kijinsia ni magumu mengine anayosimulia kama sehemu ya vikwazo ambavyo bila mapambano, pengine asingekuwa waziri anayeonekana sasa.

Dk Tax ameyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 2, 2024 alipozungumza katika uzinduzi wa Redio Malkia Choice FM inayoendeshwa na kurusha matangazo yenye maudhui ya wanawake pekee.

Anasimulia changamoto hiyo ilimkabili miaka minne baada ya kuolewa na kuwa na mtoto, wakati huo huo alipata nafasi ya masomo njema Tanzania.

“Nilijiuliza nitafanyaje kuhusu mtoto maana kusoma nataka, kumlea mwanangu nataka nilikuwa katikati. Lakini baadaye nilifanya maamuzi magumu ya kumwacha na kwenda kusoma,” amesema.

Ingawa ulikuwa uamuzi mgumu, anasema ndani yake alikuwa anafikiria mbinu gani itakayomwezesha kutengeneza mazingira ya baadaye kumchukua mwanawe ili awe naye nje ya nchi.

“Miezi sita baadaye nilifanikiwa kutengeneza mazingira na nikamchukua mwanangu na kuwa naye nje ya nchi,” amesema.

Mtihani mwingine anasema ulikuwa namna ya kutenga muda wa kusoma lakini wakati huo huo azingatie huduma za mtoto na ukizingatia alikuwa katika taifa lisilo lake.

Juhudi pekee, anaeleza ndizo zilizomwezesha kufanikisha hilo na baadaye alifaulu vema na kutakiwa kuendelea na masomo ya shahada ya uzamivu katika mazingira hayo hayo.

Baada ya mafanikio hayo, anasema kwa kuwa alishazoea mazingira mumewe pia alikwenda nchini humo na akawa anamsaidia shughuli mbalimbali zikiwemo kazi za nyumbani.

“Wanaume ni watu wa ajabu sana tulivyokuwa kule (nje ya nchi) alikuwa anafanya kila kitu lakini alivyorudi akaacha kila kitu. Nilimuuliza siku moja mbona ulipokuwa kule ulikuwa unanisaidia kila kitu hadi kutosha vyombo lakini tumerudi nchini umeacha.

“Akaniambia wewe una akili kweli? dada yangu anikute naosha vyombo atanielewaje,” anasema.

Changamoto nyingine anayosema pengine ndiyo iliyosababisha hata ateuliwe katika wizara hiyo, anasema ni uamuzi wa kupendekeza nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kujitegemea kwa vikosi vya ulinzi na usalama panapo machafuko.

“Nikiwa Katibu Mkuu wa SADC, nimekuta tunajisifu kwamba jumuiya iko vema lakini kwenye ulinzi na usalama lakini tulikuwa tegemezi wanapotaka kudeploy mission tulilazimika kuwa omba omba,” anasema.

Katika mazingira hayo, anasimulia kutengenezwa bajeti ya SADC itakayowezesha kuwa na vikosi vyao, jambo alilopata upinzani mkubwa kutoka kwa timu yake.

Anaeleza wengi walimpinga kabla hata hajalifikisha kwa wakuu wa nchi kuliwasilisha, lakini aling’ang’ana hadi alipopata nafasi ya kuliwasilisha.

“Siku nilipoliwasilisha lilipitishwa na mwaka huo ndipo tulipoanza kudeploy mission ya kwanza Misutu na Msumbiji kwa fedha za ndani,” anasema Dk Tax.

Mitihani mingine iliyowahi kumkabili, anasema ni kupewa majukumu huku akiwa haaminiki kutokana na jinsi yake, lakini amekuwa akiwashangaza wanaompa kwani alitekeleza kama ilivyotakiwa.

“Nimeivuka kwa urahisi mitihani hii kwa sababu kwanza najiamini, ninapopewa jukumu natumia juhudi na bidii kulitekeleza inavyotakiwa,” anasema.

Anaeleza changamoto iliyopo kwa baadhi ya wanawake, hupenda kujidharau na wanatanguliza udhaifu kabla hata jamii haijawatazama kwa tafsiri hiyo.

“Wewe mwenyewe unasema mimi ni mwanamke hii siiwezi badala ya kuangalia wewe daktari na mimi daktari basi naweza kama mwingine,” anasema.

Mkurugenzi wa redio hiyo, Johayna Kusaga anasema wanacholenga ni kutengeneza jukwaa linalolenga masuala ya wanawake na litajadili maudhui yanayoihusu jinsi hiyo.

“Tunatarajiwa wanaume pia watasikiliza kwa sababu sisi ni mama zao, wake zao na tumehusika katika kuhakikisha wanafika walipofika,” anasema.

Anaeleza katika redio hiyo wafanyakazi wote watakuwa wanawake na wasichana, akisisitiza haitakuwa ya kusutana kama wengine wanavyotafsiri.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA