WAANDISHI WAPEWA NONDO WATAKIWA UMAKINI KIPINDI CHA UCHAGUZI NA TAARIFA FEKI
Waandishi Watakiwa Kuwa Makini na Habari za Uchaguzi Katika Kipindi cha AI na Taarifa Feki
Tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwa makini na namna wanavyoripoti taarifa, hasa katika zama hizi za teknolojia ya akili bandia (AI) ambazo zimeongeza kasi ya kusambaa kwa taarifa za uongo, chuki na uchochezi mitandaoni.
Wito huo umetolewa katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na mpango wa #defyhatenow kupitia Global Action for Peacebuilding (GAPI) na kwa ufadhili wa GIZ. Warsha hiyo iliwaleta pamoja waandishi wa habari mbalimbali nchini na kuwapa mafunzo juu ya fact-checking, usalama wa habari mitandaoni, matumizi salama ya AI, na mbinu za kuandika taarifa zinazojenga amani wakati wa uchaguzi.
Akizungumza katika warsha hiyo, Njokii Kariuki kutoka taasisi ya Global Peace Initiative ya Nairobi, Kenya, alieleza kuwa baadhi ya taarifa huundwa kwa makusudi ili kuchochea hisia, kuharibu sifa za watu au taasisi, hasa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
“Kuna maneno yanaandikwa kwa makusudi ya kuleta taharuki au kuchochea chuki. Waandishi wanapaswa kuwa waangalifu, kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchapisha taarifa yoyote. Waulize: nani alisema? Lini? Kwa muktadha upi? Na kwa lengo gani?” amesisitiza Kariuki.
Ameongeza kuwa taarifa nyingi potofu huwasilishwa kwa kutumia muktadha wa zamani, lakini huonekana kama habari za sasa, hali inayoweza kuchangia migawanyiko ya kijamii na vurugu.
Kwa upande wake, Silvia Daulinge kutoka TAMWA amesema kuwa waandishi wanakabiliwa na changamoto kubwa katika ulimwengu wa kidijitali ambapo taarifa zisizo sahihi husambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo rasmi vya habari.
“Kumekuwa na ongezeko la hotuba za chuki na udhalilishaji, hasa dhidi ya wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi. Wanawake, vijana na makundi maalumu wana haki ya kushiriki kikamilifu bila kuonewa au kudhalilishwa,” amesema.
Silvia alisisitiza kuwa mitandao ya kijamii imefungua milango kwa kila mmoja kutoa maoni, lakini ni wajibu wa waandishi wa habari kuchambua kwa makini taarifa hizo na kuziwasilisha kwa njia inayojenga amani, si kubomoa.
“Teknolojia ya akili bandia imerahisisha utengenezaji wa picha, sauti na video bandia zinazoweza kuaminika kuwa halisi. Waandishi wanahitaji maarifa mapya ya kutambua uhalisia wa taarifa hizo,” ameongeza.
Florence Majani kutoka TAMWA naye aliwahimiza waandishi kutumia taaluma yao kama chombo cha kujenga, si cha kubomoa.
“Tunawashauri waandishi kuwa sehemu ya suluhisho. Watumie kalamu zao kujenga jamii yenye mshikamano, kuheshimu haki na usawa, na kulinda misingi ya demokrasia,” amesema.
Warsha hiyo imetajwa kuwa muhimu kwa wakati huu ambapo vyombo vya habari vinatarajiwa kuwa mhimili wa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, kwa kuhakikisha jamii inapata taarifa za haki, sahihi na zisizoegemea upande wowote.




Comments
Post a Comment