TAMWA WAZINDUA MRADI WA UFUGAJI NYUKI
TAMWA yazindua mradi wa ufugaji wa nyuk
CHAMA cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kimeanzisha mradi mpya wa ufugaji wa nyuki katika kijiji cha Msufini, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kukuza uchumi wa jamii na kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika mafunzo maalum ya ufugaji wa nyuki kwa wanachama wa TAMWA, Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Dkt. Rose Reuben amesema mradi huo unalenga kuwezesha wakazi wa Msufini kupata chanzo mbadala cha mapato kwa njia endelevu, salama na rafiki kwa mazingira.
“Tunatarajia kuwa na mizinga 200 ya nyuki katika awamu ya kwanza. Licha ya kuongeza kipato kwa familia, mradi huu utachochea uhifadhi wa mazingira kupitia matumizi ya nyuki katika misitu na bustani. Ni wakati sasa wa kuunganisha ajira, mazingira na afya ya jamii kwa njia moja,” amesema Dkt. Reuben.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023, Tanzania huzalisha tani 20 tu za asali kwa mwaka, kiwango ambacho hakitoshelezi mahitaji ya ndani. Hali hiyo imeifanya TAMWA kuona fursa ya kuwekeza kwenye sekta ya ufugaji wa nyuki kama suluhisho la kiuchumi na kijamii.
Dkt. Reuben alibainisha kuwa tayari wameanza kujenga ushirikiano na taasisi kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kusaidia kwa utaalamu na vifaa. “Tunaendelea kuwaomba wafadhili wajitokeze kuunga mkono juhudi hizi ili kupanua mradi na kuwafikia walengwa wengi zaidi,” ameongeza.
Matarajio ni kuanza rasmi kwa utekelezaji wa mradi mwezi Agosti 2025, baada ya kukamilika kwa mafunzo ya awali na usambazaji wa mizinga na vifaa vya msingi kwa wanufaika.
Kwa upande wake, Afisa Nyuki Christina Samweli amewafundisha washiriki jinsi ya kutambua asali halisi. “Asali halisi inaweza kuhifadhiwa hadi miaka miwili bila kuharibika. Unaweka maji kwenye chupa, kisha unamimina asali. Ikiwa asali inazama chini, hiyo ni halisi. Ikiwa inapanda juu, basi siyo halisi,” ameeleza.
Afisa Michechemuzi wa TAMWA, Florence Majani aliongeza kuwa mradi huu una malengo ya kuwawezesha wanawake na vijana kujiajiri, kuongeza kipato cha kaya, na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na mashirika yanayosaidia maendeleo.
“Faida za mradi huu ni nyingi – ajira, uzalishaji wa asali, uhifadhi wa mazingira na kujenga jamii yenye maarifa ya kutumia rasilimali asilia kwa uendelevu,” amesema Majani.
Kwa jamii ya Msufini, nyuki sasa si tishio tena, bali ni tumaini jipya la maendeleo.




Comments
Post a Comment