CRDB BANK FOUNDATION WAENDELEA KUWEZESHA VIJANA GO GREEN NA IMBEJU
Benki ya CRDB kwa kushirikiana na CRDB Foundation imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuwawezesha vijana kiuchumi baada ya kuchagua vijana zaidi ya 458 kuingia katika awamu ya kwanza ya mafunzo maalumu ya biashara na teknolojia kupitia programu ya Go Green na Imbeju.
Programu hiyo inalenga kuwajengea vijana uwezo katika biashara, huduma za kidijitali, uwekezaji pamoja na uchumi wa kijani ili kuwawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa kupitia shughuli endelevu zinazolinda mazingira.
Akizungumza kuhusu programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema vijana waliofanikiwa wamepatikana baada ya kupitia mchakato wa uchambuzi uliofanywa na jopo la wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi.
Mwambapa amesema vigezo vilivyotumika ni pamoja na ubunifu wa biashara, uwezo wa mradi kujiendesha pamoja na mchango wake katika kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana walionufaika na mpango huo wameeleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ujuzi wa kusimamia biashara, kutumia teknolojia katika shughuli zao pamoja na kuboresha uzalishaji.
Wameishukuru CRDB na CRDB Foundation kwa kuwapatia nafasi hiyo wakisema itakuwa chachu ya kujiajiri na pia kuajiri vijana wengine katika jamii kupitia biashara endelevu na zenye tija.





Comments
Post a Comment