IZO MOTORS YAZINDUA BETRI ZA KISASA AJIRA KWA VIJANA

IZO Motors Yazindua Betri za Kisasa, Zaajiri Zaidi ya Vijana 50 Kampuni ya IZO Motors Company Limited imesema imeendelea kuchangia kukuza ajira kwa vijana baada ya kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 50 kupitia shughuli zake za uuzaji na usambazaji wa betri pamoja na matairi kwa jumla na rejareja. Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 12, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Izo Mahenge, alisema kampuni hiyo imezindua rasmi betri mpya za izo Battery, ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na ubora wa hali ya juu kwa matumizi mbalimbali.
Mahenge amesema betri hizo zimeandaliwa kwa uwezo mkubwa wa kuhifadhi na kutoa nguvu, huku zikidumu kwa muda mrefu katika mazingira tofauti ya matumizi. “Tumetengeneza betri hizi kwa kuzingatia viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuhakikisha mtumiaji anapata bidhaa yenye ufanisi mkubwa. Biashara ni ushindani, hivyo tumejikita zaidi katika ubora na utofauti wa bidhaa yetu,” amesema Mahenge. Aidha, alieleza kuwa betri hizo zinazalishwa hapa nchini Tanzania na zina uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa muda mrefu bila changamoto, huku akiwahamasisha Watanzania kujaribu bidhaa hiyo mpya. “Kampuni yetu pia inatoa huduma ya usambazaji wa bidhaa Tanzania nzima, mijini na vijijini, kwa haraka na uhakika kulingana na mahitaji ya mteja,” ameongeza. Kwa upande wake, Balozi wa izo Battery, Dotto Magari, alisema betri hizo ni za kisasa na tofauti na baadhi ya betri za zamani kwa kuwa hazitumii maji. Amesema teknolojia hiyo mpya inalenga kuwasaidia wafanyabiashara, mafundi magari, pamoja na watumiaji wa vyombo vya moto na mashine mbalimbali kupata betri zenye nguvu na zinazodumu kwa muda mrefu. “Hizi ni betri za kisasa ambazo hazitumii maji na zina uwezo mkubwa wa kuwasha magari, jenereta, mashine za kusaga na vifaa mbalimbali vya moto. Tunawaomba wafanyabiashara na mawakala wajitokeze kushirikiana nasi kusambaza bidhaa hizi,” amesema Dotto Magari. Ameongeza kuwa matumizi ya betri hizo yatawasaidia wananchi hasa maeneo ya vijijini kupata bidhaa bora yenye uimara na ufanisi mkubwa katika kazi zao za kila siku.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA