SERIKALI YAONGEZA FURSA KWA VIJANA KUPITIA UBUNIFU WA TEKNOLOJIA USHIRIKIANO BAINA YA CRDB NA UDSM
Serikali Yaongeza Fursa kwa Vijana Kupitia Ubunifu na Teknolojia
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa fursa kwa vijana nchini zinaendelea kuongezeka, hasa kwa wale wenye ubunifu na uwezo wa kubuni suluhisho za changamoto mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi wa IMBEJU – UDSM Startup Challenge 2026, Prof. Mkenda amesema kuwa programu hiyo ni sehemu muhimu ya juhudi za serikali katika kutekeleza ajenda ya kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia ubunifu na teknolojia.
Ameeleza kuwa kupitia mashindano hayo, vijana watapata nafasi ya kuendeleza mawazo yao ya kibiashara, kupata msaada wa kitaalamu pamoja na uwezeshaji utakaowasaidia kujenga maisha bora na kujiajiri.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya vitendo kupitia vyuo vya ufundi na vyuo vikuu, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye, aliwasihi vijana kutumia fursa wanazozipata kwa kuweka uzalendo mbele pamoja na kuzingatia maadili katika kuzitumia.
Prof. Anangisye ameeleza kuwa ipo haja kwa wanafunzi na wahitimu kushirikiana kwa karibu katika kutafuta suluhisho la changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu, akibainisha kuwa fursa kama hizi ni za kipekee na zinapaswa kutumika ipasavyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, aliwasihi vijana wa UDSM kuweka uzalendo mbele na kuzingatia maadili katika kutumia fursa wanazozipata.
Mwambapa ameeleza kuwa kupitia programu ya IMBEJU – UDSM Startup Challenge, wanatarajia kuwezesha angalau ubunifu (startups) 100 ambazo zitachangia moja kwa moja kuunda ajira kwa zaidi ya vijana 500.
Aidha, amebainisha kuwa kuna takribani mawazo 30 yenye ubunifu mkubwa yatakayoweza kuingia sokoni mara moja.









Comments
Post a Comment