BALOZI KIBESSE WASANII TANGAZENI KISWAHILI KIMATAIFA KUPITIA SANAA
Balozi Kibesse awataka wasanii kutangaza Kiswahili kimataifa kupitia sanaa
Na Brigitte
Nairobi, Kenya
BALOZI wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Bernard Kibesse, amewataka wasanii wa Tanzania kuendelea kutumia sanaa zao kutangaza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Dkt. Kibesse ametoa kauli hiyo jijini Nairobi baada ya kukutana na wasanii waliotembelea ubalozi wa Tanzania nchini humo, mara baada ya kushiriki Kongamano la The East African Art Nexus (TEANEX).
Amesema sekta ya sanaa ni miongoni mwa sekta zinazopendwa na watu wa rika zote, hivyo ina nafasi kubwa ya kuitangaza Kiswahili kwa kasi kupitia muziki, filamu na sanaa za maonyesho.
“Sekta ya sanaa inapendwa na watu wa kila rika, hivyo kupitia burudani, Kiswahili kinaweza kusambaa kwa haraka zaidi ndani na nje ya Tanzania,” amesema Dkt. Kibesse.
Ameongeza kuwa wasanii wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa kueneza Kiswahili, pamoja na kuonesha upendo na amani iliyopo nchini Tanzania kupitia kazi zao za sanaa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutangaza utamaduni wa Kitanzania, ikiwa ni pamoja na mila na desturi, wanapokuwa katika mataifa mbalimbali duniani.
“Utamaduni wetu, mila na desturi ni msingi wa taifa letu, tusisite kuutangaza tunapokuwa nje ya nchi,” amesisitiza.
Pia, amewakaribisha Watanzania wote watakaofika nchini Kenya kutembelea ubalozi huo, akieleza kuwa ni mahali pao salama na nyumbani kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Rais wa Sanaa za Ufundi, Andrian Nyangamale, ameishukuru Serikali kupitia ubalozi huo kwa mapokezi mazuri waliyoyapata wasanii hao walipofika Nairobi.
Kongamano la TEANEX lililowakutanisha wasanii kutoka Afrika Mashariki lililenga kujenga jukwaa la pamoja litakalowaunganisha wasanii hao ili kuwa na sauti moja katika kuleta mabadiliko na kutambulika zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.










Comments
Post a Comment