WAZIRI KAPINGA AIPONGEZA CRDB KWA KUWAINUA WAJASIRIAMALI
Waziri Kapinga aipongeza CRDB kwa kuinua wajasiliamali, kuchochea uchumi wa wanawake
DAR ES SALAAM:WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameipongeza CRDB Bank kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu katika kukuza maendeleo ya wajasiriamali nchini kupitia utoaji wa elimu ya fedha na fursa za mitaji.
Akizungumza katika hafla ya Kitchen Party Gala 2026, ambapo CRDB ilikuwa mdhamini, Waziri Kapinga alisema mchango wa taasisi za kifedha ni muhimu katika kujenga uchumi imara na jumuishi.
“Jamii yetu inahitaji maendeleo ya uhakika ya uchumi ili kukabiliana na umasikini pamoja na changamoto nyingine. Ili kufanikisha hili, ushiriki wa kila mmoja ni muhimu. Nawapongeza CRDB na wadhamini wengine kwa kufanikisha hafla ya mwaka huu. Wanawake ni chemchem ya mafanikio ya familia,” amesema.
Katika hafla hiyo, CRDB ilitoa elimu ya fedha pamoja na kuwasilisha fursa mbalimbali za kukuza mitaji kwa wajasiriamali wachanga na wadogo, hatua inayolenga kuwaongezea uwezo wa kifedha, kuboresha usimamizi wa biashara zao na kuongeza ushindani sokoni.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Biashara Changa na Ndogo wa CRDB, Agness Kisinini, amesema wanawake wenye kipato halali na uchumi imara ni msingi muhimu wa familia na taifa kwa ujumla.
“Benki yetu ina akaunti na bidhaa mahsusi kwa ajili ya mwanamke wa shoka. Nawasihi kutumia huduma hizi ili kufanikisha safari zenu za kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa ushiriki wa benki hiyo katika jukwaa hilo unalenga kuimarisha ujumuishi wa kifedha kwa kuwafikia wajasiriamali katika sekta bunifu na zinazoibukia, pamoja na kuongeza uelewa wa huduma za kifedha zinazochochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa nidhamu ya fedha, uwekezaji sahihi na matumizi ya huduma rasmi za kifedha kama msingi wa mafanikio ya muda mrefu kwa wajasiriamali.
CRDB Bank imeendelea kuamini kuwa majukwaa kama Kitchen Party Gala si tu yanaonesha ubunifu, bali pia ni daraja muhimu la kuwapatia wajasiriamali maarifa, mitandao na rasilimali zinazohitajika kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.







Comments
Post a Comment