NANCY SUMARI: MREMBO ANAYELETA MAPINDUZI SEKTA YA ELIMU KALIMANI APP
Nancy Sumari: Kutoka Urembo hadi Mapinduzi ya Elimu ya Kidijitali kwa Watoto Viziwi
WENGI wanamkumbuka Nancy Sumari kama mrembo aliyewahi kutwaa taji la Miss Tanzania 2006 na baadaye kutangaza jina la nchi kimataifa kupitia Miss World Africa.
Lakini leo, anajitokeza upya si kwa urembo bali kwa mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu jumuishi kupitia teknolojia.
Kupitia kampuni yake ya JengaHub, Nancy amezindua rasmi Kalimani App, jukwaa la kidijitali linalolenga kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa kusikia kujifunza kwa urahisi zaidi, popote walipo.
Teknolojia Inayogusa Maisha
Akizungumza na Amonline jijini Dar es Salaam, Nancy alisema kuwa programu hiyo imetengenezwa kwa kusaidia watoto viziwi.
“Kalimani App inatumia lugha ya alama ya Tanzania kufundisha kusoma, kuandika na kuhesabu, pamoja na kuwajengea watoto ujuzi wa kidijitali,” ameeleza.
Programu hiyo inatarajiwa kuanza kutumika katika shule za kawaida na maalum katika mikoa sita nchini, hatua inayolenga kupunguza pengo la elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Kutambulika Kimataifa
Ubunifu huo tayari umeanza kuipa Tanzania heshima duniani.
Februari 2026, Nancy alishinda tuzo ya ubunifu kutoka Zero Project nchini Austria, tuzo iliyotolewa jijini Vienna.
Kalimani App ilichaguliwa miongoni mwa miradi bora inayochochea elimu jumuishi duniani, ikiiwakilisha Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa.
Ushirikiano wa Ndani Kuimarisha Elimu
Maendeleo ya programu hiyo yamehusisha ushirikiano wa karibu na taasisi mbalimbali ikiwemo Child Support Tanzania na Kyaro Assistive Tech, pamoja na wadau wakuu wa elimu nchini.
Kupitia ushirikiano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), maudhui ya Kalimani App yameandaliwa kwa kuzingatia mitaala rasmi ya elimu.
“Tulishirikiana na walimu na wataalamu wa elimu kuhakikisha tunakidhi mahitaji halisi ya watoto viziwi,” amesema Nancy.
Maboresho ya Somo la Hesabu
Katika hatua nyingine muhimu, TET kwa kushirikiana na JengaHub imeanza kuboresha maudhui ya somo la hesabu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu, kwa lengo la kuwajumuisha watoto viziwi katika mfumo wa elimu.
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Aneth Komba, alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha maudhui yanawafikia watoto wote bila ubaguzi.
“Tunapitia na kuhuisha mitaala ili iweze kuwafikia watoto wenye ulemavu wa usikivu kwa ufanisi zaidi,” ameeleza.
Kupitia Kalimani App, watoto hao wataweza kujifunza hesabu kwa njia rafiki, kwa kutumia picha, video, sauti na vielelezo vinavyorahisisha uelewa.
Mradi wa Kalimani
Jitihada hizo zinaendeshwa chini ya mradi wa huo, unaolenga kutumia teknolojia kuboresha uwezo wa watoto wenye mahitaji maalum kumudu stadi za msingi za hesabu.
Nancy alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma kielimu, sambamba na sera ya elimu jumuishi inayosisitizwa na serikali.
Safari ya Mabadiliko
Kabla ya ubunifu huu wa kidijitali, Nancy pia alijikita katika uandishi wa vitabu vya watoto, ikiwemo Nyota Haiki, akilenga kuwahamasisha watoto kujisomea.
Wazo la Kalimani App lilizaliwa baada ya kubaini changamoto kubwa kwa watoto viziwi kushindwa kufuatilia masomo darasani kutokana na ukosefu wa lugha ya alama.
Teknolojia Kama Suluhisho
Nancy anaamini kuwa teknolojia ni daraja muhimu kati ya changamoto na suluhisho katika elimu.
“Mwalimu na mzazi wanaweza kutumia mfumo huu bure kuboresha uelewa wa mtoto. Tuko tayari pia kutoa mafunzo ya matumizi yake,” amesema.
Chachu ya Mabadiliko
Kupitia Kalimani App, Nancy Sumari anaendelea kuthibitisha kuwa ubunifu wa Kitanzania unaweza kuleta mabadiliko makubwa ndani na nje ya nchi.
Zaidi ya kuwa suluhisho la elimu, jukwaa hilo linafungua milango ya fursa mpya kwa watoto viziwi katika dunia ya kidijitali likiwa ni hatua muhimu kuelekea Tanzania jumuishi zaidi.
Wito kwa wazazi
Nancy, ambaye pia ni mzazi, amesema teknolojia inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kusaidia walimu na wazazi katika kuboresha uelewa wa watoto wenye mahitaji maalum darasani na nyumbani.
“Sisi kama wabunifu wa masuala ya teknolojia tumeona hii ni fursa ya kuweza kuwasapoti watoto viziwi. Mwalimu anayefundisha wanafunzi viziwi anaweza kutumia platform yetu ambayo ni bure kuweza kuimarisha uelewa wa masomo, kuimarisha ufahamu na ushiriki wa wanafunzi,” amesema.
Ametoa wito kwa wazazi na walimu kutumia fursa hiyo ya teknolojia kwa manufaa ya watoto, huku akisisitiza kuwa Jenga Hub iko tayari kutoa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huo.


















Comments
Post a Comment