WAWEKEZAJI WATAKIWA KUTUMIA HUDUMA ZA TBS KUIMARISHA UBORA WA BIDHAA
Wawekezaji Watakiwa Kutumia Huduma za TBS Kuimarisha Ubora wa Bidhaa
DAR ES SALAAM:
Wito umetolewa kwa wawekezaji na wazalishaji nchini kutumia huduma za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hususan katika sekta ya vipimo (metrolojia), kufuatia kutambulika kwake kimataifa.
Akizungumza na wanahabari Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Metrolojia wa TBS, Joseph Kadenge, amesema kuwa metrolojia—yaani sayansi ya vipimo—ni moja ya nguzo nne muhimu za ubora, inayohakikisha usahihi wa vipimo katika mashine zinazotumika kwenye uzalishaji.
Ameeleza kuwa ubora wa bidhaa huanza moja kwa moja na ubora wa mashine zinazozalisha bidhaa hizo. Endapo mashine hazitakuwa na vipimo sahihi, basi hata bidhaa zinazozalishwa zitakosa ubora unaotakiwa.
Kadenge ameongeza kuwa TBS inamiliki Maabara ya Taifa ya Vipimo (National Metrology Laboratory) ambayo imetambulika kimataifa kupitia Shirika la Vipimo Duniani (BIPM), huku uwezo wake wa upimaji ukiwa umeorodheshwa katika kanzidata ya kimataifa.
Aidha, maabara hiyo imepata ithibati ya umahiri kutoka SADCAS, taasisi ya kikanda inayohusika na uthibitishaji wa viwango vya ubora katika nchi za SADC. Hatua hiyo inathibitisha ubora wa huduma zinazotolewa na TBS na kuwapa uhakika wawekezaji kuhusu viwango vinavyotumika.
Kutokana na mafanikio hayo, Kadenge amewahimiza wawekezaji na wazalishaji kutokuwa na hofu ya kuwekeza nchini Tanzania, akisisitiza kuwa huduma za ugezi (calibration) zinapatikana kwa urahisi na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.



Comments
Post a Comment