SERIKALI YAIMARISHA USIMAMIZI NGUMI ZA KULIPWA KULINDA MABONDIA
Serikali Yaimarisha Usimamizi wa Ngumi za Kulipwa Kulinda Maslahi ya Mabondia
Na Brigitte
DAR ES SALAAM: Serikali imesisitiza kuendelea kuweka mkazo katika usimamizi wa mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, ikiwa ni jitihada za kulinda maslahi ya mabondia na kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha vijana kiuchumi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tovuti ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya uratibu na kudhibiti masuala ya mchezo huo ili kuondoa changamoto zilizokuwa zikikwamisha maendeleo yake.
Ameeleza kuwa uwepo wa tovuti hiyo utaongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika sekta ya ngumi, huku ukiwasaidia wadau kufuatilia taarifa muhimu kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya TPBRC, Patrick Nyembera, alisema kamati hiyo imebaini changamoto mbalimbali katika kipindi cha utekelezaji wa majukumu yake, zikiwemo baadhi ya mabondia kunyimwa haki zao za msingi kama malipo ya kazi zao.
Ameongeza kuwa pia kumekuwepo na vitendo vya baadhi ya watu kuwatumia mabondia kujipatia fedha bila ridhaa yao, kuwasafirisha nje ya nchi kinyume cha sheria, pamoja na kughushi nyaraka za kamisheni kwa lengo la kufanikisha vitendo hivyo.
“Tutawasilisha taarifa rasmi kwa serikali ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema Nyembera, akisisitiza kuwa tovuti hiyo itasaidia kudhibiti changamoto hizo.
Naye Msitha alionya kuwa serikali haitavumilia ukiukwaji wa taratibu na sheria, akibainisha kuwa tayari hatua zinaanza kuchukuliwa dhidi ya wanaotuhumiwa kuwatumia vibaya mabondia, ikiwemo kuwasafirisha nje ya nchi kinyume cha sheria.
Aidha, amewataka wadau wa mchezo huo kubadilika na kuunga mkono mabadiliko yanayolenga kuimarisha sekta hiyo, akisisitiza kuwa mifumo mipya itaongeza uwazi na uwajibikaji kwa manufaa ya wote.





Comments
Post a Comment