BASATA YACHOCHEA UCHUMI WA UBUNIFU KUPITIA MASHINDANO YA UCHORAJI
BASATA yachochea Uchumi wa Ubunifu kupitia mashindano ya Uchoraji kwa Wanafunzi
Na Brigitte
DAR ES SALAAM:KAIMU Katibu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga, amesema mashindano ya uchoraji yanayoshirikisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini ni mkakati muhimu wa kukuza, kuinua na kuendeleza vipaji vya sanaa sambamba na kuchangia uchumi wa ubunifu nchini.
Akizungumza na Amonline Edward Buganga ameeleza kuwa BASATA itaendelea kuandaa mashindano hayo ili kuwapa vijana jukwaa la kuonesha ubunifu wao na kukuza taaluma ya sanaa.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza atajinyakulia shilingi laki tano, mshindi wa pili shilingi laki tatu, na mshindi wa tatu shilingi laki moja. Washindi wote pia watapatiwa vyeti pamoja na vifaa vya kuchorea ili kuwasaidia kuboresha kazi zao za sanaa.
Aidha, Buganga amebainisha kuwa mashindano ya muziki yanaendelea kupokea kazi za washiriki, huku BASATA ikiwa katika mipango ya kuanzisha mashindano ya sarakasi ili kupanua zaidi wigo wa sanaa nchini.
Katika hatua ya kuimarisha sanaa za picha nchini, BASATA imeanzisha mashindano hayo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hususa ni kupitia Idara ya Sanaa za Ubunifu, ambayo imekuwa kitovu cha kuibua vipaji na wajasiriamali wa sanaa.
Buganga amesisitiza kuwa uchoraji ni nyenzo muhimu katika kuwasilisha ujumbe wa kijamii, kukuza ubunifu na kuendeleza vipaji vya vijana.
Ameeleza kuwa malengo makuu ya mashindano hayo ni kubaini na kukuza vipaji vya sanaa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, kuwapa fursa ya kuonesha ubunifu wao, pamoja na kuongeza thamani ya sanaa katika jamii na taasisi za elimu ya juu. Pia mashindano hayo yanahamasisha wanafunzi kujituma zaidi na kuwajengea msingi wa kujiajiri kupitia sanaa.
Buganga, BASATA kwa kushirikiana na wadau imeandaa mwongozo maalum wa mashindano ya uchoraji unaolenga kuhakikisha ubora, uwazi na haki kwa washiriki wote.
"Mwongozo huo unazingatia ubunifu wa asili, ustadi wa kiufundi pamoja na mchango wa kazi za sanaa katika kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa taifa.
Ameongeza kuwa sekta ya sanaa ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kwa kuwawezesha vijana kujiajiri, kuongeza kipato na kuitangaza nchi kimataifa kupitia kazi za ubunifu.
“Ni muhimu kwa wanafunzi kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano haya kwani ni fursa adhimu ya kukuza vipaji na kujenga mustakabali wao,” amesisitiza Buganga, huku akitoa shukrani kwa uongozi wa UDSM na washiriki wote kwa kufanikisha mashindano hayo.
Kwa upande wake, Gift Lwemamu, mwanafunzi wa sanaa kutoka UDSM, ameshukuru BASATA kwa kuwapatia vifaa vya kuchorea akisema vitarahisisha kazi zao na kuongeza ubunifu.
Naye Julius Pallanjo amesema mashindano hayo yanasaidia kuinua vipaji vya wanafunzi na kuwajengea ujuzi kupitia ushindani, jambo linalowasaidia kukua kisanaa na kitaaluma.







Comments
Post a Comment