CRDB BANK YANGARA TUZO KIMATAIFA
BENKI ya CRDB Bank imepata heshima ya kutambuliwa kimataifa baada ya kushinda tuzo ya benki bora katika utoaji wa huduma za kifedha kwa wateja maalum (Private Banking) kutoka kwa Euromoney, hatua inayodhihirisha ukuaji wa sekta ya fedha nchini Tanzania.
Akizungumza leo Aprili, 21 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dk. AbdulMajid Nsekela, amesema mafanikio hayo yanaweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuaminika zaidi kimataifa.
Ameeleza kuwa ushindi huo unasaidia kuongeza imani kwa wawekezaji wa ndani na nje.
“Tuzo hii inaonyesha uimara wa mifumo ya kifedha nchini, hali inayochochea wawekezaji wengi zaidi kuichagua Tanzania kama sehemu salama ya kuwekeza na kuhifadhi mitaji yao,” amefafanua Dk. Nsekela.
Aidha, amesema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi madhubuti wa sekta ya fedha unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Wizara ya Fedha Tanzania, ambazo zimeweka sera rafiki zinazokuza ubora wa huduma za kifedha.
Ameongeza kuwa maendeleo ya teknolojia ya kifedha yameongeza urahisi wa wananchi na wafanyabiashara kutumia huduma za benki bila kubeba fedha taslimu, jambo linalosaidia kuongeza usalama na ufanisi katika miamala.





Comments
Post a Comment