TBS YAADHIMISHA MIAKA 50 KWA MATUKIO MAKUBWA YA KITAIFA

TBS Yaadhimisha Miaka 50 kwa Matukio Makubwa ya Kitaifa ya Ubora na Usalama
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linatarajia kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 kwa kuandaa matukio mbalimbali makubwa ya kitaifa, yakiwemo Viwango Marathon, Viwango Business Forum pamoja na Gala Dinner maalum ya usiku wa Jubilei hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema maadhimisho hayo yanaakisi mafanikio makubwa ambayo taasisi hiyo imeyapata katika kipindi cha nusu karne ya kusimamia ubora, usalama wa bidhaa na huduma nchini. TBS ilianzishwa mwaka 1975 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake mwaka 1976 chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Sheria ya Viwango Sura ya 130, ikiwa sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha sekta ya viwanda na biashara nchini. Katika kipindi cha miaka 50, TBS imeendelea kuwa mhimili muhimu wa kulinda afya na usalama wa walaji, kukuza ushindani wa bidhaa za ndani pamoja na kuwezesha wazalishaji wa Tanzania kufikia masoko ya kikanda na kimataifa kupitia mifumo ya viwango vinavyotambulika duniani. Kadri uchumi wa Tanzania ulivyokuwa ukikua na mahitaji ya soko kubadilika, shirika hilo limepanua wigo wa huduma zake na kuwa taasisi yenye mchango mkubwa katika sekta za viwanda, biashara, afya ya jamii na maendeleo ya teknolojia. Mafanikio ya TBS yameonekana katika maeneo mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, kuongezeka kwa umahiri wa maabara, maendeleo ya TEHAMA pamoja na kutambulika kimataifa katika masuala ya viwango na uthibitishaji wa ubora.
Akizungumzia maadhimisho hayo, Dkt. Katunzi amesema miaka 50 ni hatua kubwa inayostahili kutambuliwa kwa heshima kubwa huku ikiwa ni nafasi ya taasisi hiyo kujitathmini na kuweka mikakati madhubuti ya kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi katika miaka ijayo. Katika kuenzi historia hiyo, TBS pia inatarajia kuzindua kitabu maalum kitakachoelezea safari ya shirika hilo, mafanikio yake katika kipindi chote cha utendaji kazi pamoja na maono yake kwa wadau na Watanzania kwa ujumla. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Miaka 50 ya Kuchochea Ubora na Usalama kwa Maisha Bora,” ikiwa ni dhamira ya TBS kuendelea kusimamia viwango kwa maendeleo ya taifa. Matukio ya Jubilei ya Miaka 50 ya TBS TBS imesema Viwango Marathon itafanyika Mei 23, 2026 katika Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamasisha afya na matumizi ya bidhaa zilizothibitishwa ubora wake. Aidha, Viwango Business Forum itafanyika Juni 5, 2026 katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, ambapo wafanyabiashara, wawekezaji, wazalishaji pamoja na wataalam wa viwango watapata fursa ya kujadili namna ya kukuza biashara kupitia viwango vya kimataifa. Siku hiyo hiyo kutafanyika Gala Dinner ya Jubilei ya Dhahabu katika Ukumbi wa Mlimani City kwa lengo la kutoa shukrani kwa watumishi wa zamani na wa sasa waliotoa mchango mkubwa katika mafanikio ya TBS. Kupitia programu ya Kurudisha kwa Jamii (CSR), TBS pia itatoa msaada kwa hospitali yenye uhitaji maalum Juni 16, 2026 kama sehemu ya kuunga mkono huduma za jamii. Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Juni 19, 2026 ambapo viongozi wa Serikali, sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa biashara watakutana kusherehekea mafanikio ya miaka 50 ya TBS na kuweka dira ya maendeleo kwa miaka ijayo. TBS imewataka wadau na wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki na kudhamini matukio hayo muhimu yatakayotoa nafasi ya kujifunza, kujenga mitandao ya kibiashara pamoja na kutangaza huduma na bidhaa mbalimbali. “Maadhimisho haya kwetu ni miaka 50 ya kiviwango, miaka 50 ya ushindi,” imeeleza TBS.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA