WAGONJWA WA UNENE KUPITA KIASI KUPATA MATIBABU YA KITAALAMU
Wagonjwa wa unene kupita kiasi sasa kupata huduma za kisasa za kitaalamu
Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imezindua rasmi Kliniki ya Kisasa ya Uzito Uliopitiliza (Comprehensive Obesity Clinic), hatua inayolenga kusaidia wananchi kudhibiti uzito na kuboresha afya zao kupitia huduma za kitaalamu na za fani mbalimbali.
Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam, ambapo hospitali hiyo ilieleza kuwa kliniki hiyo imeanzishwa kutokana na ongezeko la changamoto ya uzito uliopitiliza na magonjwa yanayotokana na hali hiyo.
Kliniki hiyo inawakutanisha wataalamu wa afya kutoka nyanja mbalimbali, wakiwemo madaktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, moyo, mfumo wa homoni pamoja na wataalamu wa lishe, kwa lengo la kutoa huduma jumuishi zinazolingana na mahitaji ya kila mgonjwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Masolwa Ngwanasayi amesema uzito uliopitiliza una uhusiano mkubwa na ugonjwa wa mafuta kwenye ini (fatty liver disease), hali inayotokana na changamoto za kimetaboli na mmeng’enyo wa chakula.
Ameeleza kuwa wagonjwa wanahitaji tathmini ya kina ya kitabibu ili kupata matibabu sahihi kulingana na hali zao binafsi.
Kwa upande wake, Dkt. Nadeem Kassam amesema uzito uliopitiliza huongeza hatari ya kupata shinikizo la damu, ugonjwa wa mishipa ya moyo, moyo kushindwa kufanya kazi pamoja na kiharusi.
“Matibabu ya mapema, uchunguzi wa mara kwa mara na mabadiliko ya mtindo wa maisha ni muhimu katika kuzuia madhara ya muda mrefu ya moyo,” amesema.
Naye Dkt. Hanifa Mbithe ameeleza kuwa changamoto ya uzito uliopitiliza inahusiana kwa karibu na hitilafu za homoni na michakato ya kimetaboli mwilini.
Amesema hali hiyo huathiri namna mwili unavyohifadhi mafuta, kudhibiti hamu ya kula na mwitikio wa mwili katika mabadiliko ya mtindo wa maisha, hivyo kuhitaji uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini chanzo halisi cha tatizo.
Kwa upande wa lishe, Louiza Shem alisema unene ni ugonjwa unaochangiwa na sababu nyingi, zikiwemo mazingira na tabia za ulaji.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango endelevu wa lishe bora unaozingatia mtindo wa maisha, utamaduni na aina ya vyakula vinavyopatikana kwa mgonjwa.
“Udhibiti wa uzito si ukamilifu, bali ni safari ya maendeleo ya maisha yote,” amesema.
Kliniki hiyo itatoa huduma mbalimbali za kisasa zikiwemo:Matibabu ya mfumo wa chakula na homoni, Uwekaji wa puto maalum tumboni (intragastric balloon)
Upasuaji wa kupunguza tumbo la chakula (bariatric surgery)Dawa za kusaidia kudhibiti uzitoHospitali hiyo ilieleza kuwa kila mgonjwa atafanyiwa tathmini ya kina ili kuandaliwa mpango maalum wa matibabu unaoendana na historia yake ya afya, mtindo wa maisha na malengo ya kiafya.
Kupitia uzinduzi wa kliniki hiyo, Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam imeendelea kuonesha dhamira yake ya kutoa huduma za kisasa, jumuishi na zinazomweka mgonjwa mbele katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na uzito uliopitiliza.





Comments
Post a Comment