AIRTEL YAZINDUA HUDUMA KUPAMBANA NA MATAPELI TANZANIA

Airtel Yazindua Huduma Kupambana na Utapeli Tanzania Dar es Salaam, Airtel Tanzania leo imezindua huduma mpya inayotumia teknolojia ya Akili Mnemba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya utapeli wa mitandaoni nchini. Huduma hiyo, inayojulikana kama Airtel Spam Alert - Kataa Matapeli, inalenga kuwatahadharisha wateja kuhusu jumbe za kitapeli kupitia simu janja na simu za kawaida bila hitaji la kupakua programu yoyote.
Huduma hiyo imeanzishwa kufuatia mafanikio yaliyopatikana nchini Nigeria na Uganda, ambapo Airtel imekuwa ikiboresha huduma zake za kulinda wateja dhidi ya ulaghai. Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry Silaa, aliipongeza Airtel kwa hatua hiyo,
"Huduma ya Airtel Spam Alert - Kataa Matapeli, inayotumia Akili Bandia kugundua ulaghai mtandaoni, inaendana na juhudi za serikali za kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya matapeli wa simu," amesema. Waziri Silaa ameongeza kuwa huduma hiyo inaunga mkono kampeni ya kitaifa dhidi ya udanganyifu wa simu za mkononi inayojulikana kama Sitapeliki, ambayo inalenga kuelimisha umma na kuwasaidia kutambua na kuepuka matapeli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amesema kuwa huduma hiyo mpya ni sehemu ya dhamira ya kampuni katika kulinda wateja wake dhidi ya vitisho vya kidijitali. "Huduma ya 'Airtel Spam Alert' Kataa Matapeli siyo tu hatua muhimu ya kiteknolojia, bali pia ni tamko kwamba Airtel Tanzania ni mlezi wa kidijitali wa wateja wake.
"Tunaendelea kujitahidi kuwawezesha wateja wetu kuwa makini na kufurahia manufaa ya mawasiliano ya kidijitali kwa usalama zaidi," amesema Kamoto. Kamoto pia alitoa wito kwa wadau wa sekta ya mawasiliano kushirikiana katika mapambano dhidi ya utapeli wa simu kwa ajili ya kulinda jamii.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA