WADAU WAOMBWA KUJITOKEZA KUDHAMINI MAOMBI YA UCHAGUZI MKUU
Wadau Watakiwa Kujitokeza Kudhamini Tamasha la Kuombea Uchaguzi Mkuu
Wadau mbalimbali na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kujitokeza kwa wingi kudhamini Tamasha la Kuombea Uchaguzi Mkuu, ambalo litafanyika katika mikoa 26 nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mnamo Aprili 2, Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion, Alex Msama, alisema tamasha hilo halitakuwa na kiingilio ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki katika kuliombea taifa. Aidha, alibainisha kuwa maandalizi yanaendelea vizuri.
Msama alieleza kuwa tamasha hilo litaanzia katika mkoa wa Dar es Salaam na baadaye kuendelea katika mikoa mingine, llikiwashirikisha wachungaji na maaskofu kutoka maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanaiombea amani nchi kuelekea uchaguzi mkuu.
Pia, alisema waimbaji mbalimbali maarufu kutoka ndani na nje ya nchi watashiriki katika tamasha hilo la kipekee.
"Tutatangaza tarehe na eneo rasmi la kufanyika kwa tamasha hili hivi karibuni kwa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo ndiko litakapoanzia," amesema Msama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makanisa ya Pentekoste mkoa wa Dar es Salaam, Mchungaji Emmanuel Mwasota, alisema tamasha hilo linalenga kuwaunganisha waumini wa madhehebu yote kwa ajili ya kuiombea nchi, viongozi, wabunge, madiwani na Rais ili uchaguzi upite kwa amani.
"Sisi tumeamua kushikamana kwa pamoja, na tunahakikisha taarifa hizi zinafika kila mahali kwa makanisa, wachungaji, maaskofu na wahubiri wa aina mbalimbali. Tutaungana kwa ajili ya kuiombea nchi yetu ipite salama kwenye uchaguzi utakaofanyika mwaka huu," alisema Mwasota.
Aliongeza kuwa uchaguzi unaweza kusababisha migawanyiko ikiwa raia hawatakuwa wazalendo na kuthamini amani. Kwa mantiki hiyo, aliwasihi Watanzania kushiriki kikamilifu katika maombi haya ili kuhakikisha taifa linapitia kipindi cha uchaguzi kwa utulivu na mshikamano.

Comments
Post a Comment