BOLT YAZINDUA HUDUMA SCHEDULED RIDES
Bolt Yazindua Huduma ya "Scheduled Rides" na Ufuatiliaji wa Safari za Ndege kwa Ufanisi Zaidi
Dar es Salaam, Tanzania – 30 Aprili 2025
Katika juhudi za kuendelea kuboresha huduma zake za usafiri nchini Tanzania, kampuni ya Bolt imezindua dirisha jipya la kupanga safari mapema (Scheduled Rides), sambamba na huduma ya kisasa ya kufuatilia safari za ndege (Flight Tracking), hatua inayolenga kuongeza ufanisi na urahisi kwa watumiaji wake.
Kuanzia jana, wateja wanaotumia programu ya Bolt sasa wanaweza kupanga safari zao za usafiri mapema kwa urahisi kupitia kitufe cha “Schedule” kwenye app.
Hii ni sehemu ya maboresho ya kidijitali yanayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza usumbufu kwa wasafiri, hasa wale wanaoelekea au kutoka uwanja wa ndege.
Akizungumza kuhusu huduma hiyo mpya, Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania na Kenya, alisema:
"Teknolojia inabadilika kwa kasi na Bolt inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuleta ubunifu unaotatua changamoto halisi za wasafiri. Huduma ya Flight Tracking ni suluhisho la kisasa kwa wateja wanaosafiri kwa ndege, hasa wakati ndege yao inachelewa au kufutwa. App itasasisha muda wa kuchukuliwa kiotomatiki au kufuta safari bila gharama yoyote ya ziada."
Kwa kutumia huduma hii mpya, wateja wanaweza kuweka maelezo ya safari ya ndege kama sehemu ya mchakato wa kupanga usafiri kupitia app ya Bolt. Ikiwa ndege itachelewa au kubadilishwa, muda wa kuchukuliwa utarekebishwa moja kwa moja bila kuathiri safari yao.
"Kwa mfano, katika nchi kama Ufaransa na Poland, huduma hii tayari inawawezesha wateja kupanga magari ya Bolt kwa vikundi kupitia mashirika ya ndege au mamlaka za miji. Hapa Tanzania, tunaleta teknolojia hiyo ili kusaidia abiria wanaowasili katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere bila kero ya kutafuta usafiri." aliongeza Dimmy.
Bolt sasa inatoa huduma ya usafiri katika zaidi ya viwanja vya ndege 30 duniani kote. Kupitia huduma hizi mpya, kampuni inalenga kuchangia katika mapinduzi ya kidijitali kwenye sekta ya usafiri nchini Tanzania.

Comments
Post a Comment