MSANII CHEMICAL SASA NI DKT LUBAO
Msanii Chemical apata shahada ya udaktari: “Nimeamka Kama Dkt. Lubao!”
Kwa muda mrefu, wasanii wamekuwa wakitazamwa kama watu waliopungukiwa na elimu ya juu. Lakini msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Claudia Lubao maarufu kama Chemical, amevunja dhana hiyo kwa kishindo baada ya kufanikiwa kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha St Andrews, Uingereza.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dr. Lubao alitangaza habari hiyo njema kwa mashabiki wake akieleza kuwa amefanikisha mtihani wa mwisho wa Viva, hatua ya mwisho kabla ya kutunukiwa shahada hiyo ya heshima.
"Niliwahi kuwa na ndoto… na leo, nimeamka kama Dkt. Lubao! Najihisi kuheshimiwa sana na nina shukrani za dhati kwa msaada mkubwa nilioupata kutoka kwa wasimamizi wangu, idara nilizoshirikiana nazo, marafiki, muziki wangu, na familia yangu ya mtandaoni," aliandika.
St Andrews ni miongoni mwa vyuo vikongwe na vinavyoheshimika zaidi barani Ulaya, na mafanikio ya Dr. Lubao yanamweka katika kundi adimu la wasanii wa Afrika waliotunukiwa shahada ya udaktari, na zaidi ni alama ya uwezeshaji kwa wanawake wanaojitahidi kung’ara kwenye kila nyanja – kutoka kwenye jukwaa la muziki hadi kwenye ukumbi wa mihadhara.
Msanii huyo ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza usawa wa kijinsia na haki za kijamii kupitia hip-hop, amesema amefanikisha hatua hiyo kwa msaada wa taasisi kama Earth Sciences STA, SGSD St Andrews, Laidlaw Music Centre, Urithi Wetu, na wengineo.
Wakati sasa akiwa amejiunga na orodha ya wasanii waliobobea kitaaluma kama Nikki wa Pili na Mwana FA – ambao pia ni viongozi wa serikali – Dr. Lubao anabaki kuwa mfano bora kwa vijana, hasa wa kike, kuwa ndoto zinaweza kufikiwa bila kuacha vipaji au misimamo yao.
Tunampongeza Dr. Lubao kwa mafanikio haya makubwa ya kihistoria.


Comments
Post a Comment