GWAJIMA AWATAKA WANAWAKE KUJIUNGA MAJUKWAA YA KIUCHUMI
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wanawake kujiunga na Majukwaa ya Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi Ili kuzifahamu fursa za kiuchumi zilipo nchini.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Aprili 08, 2025 jijini Dar Es Salaam wakati akipokea nakala 1000 za Mwongozo wa Uundaji na Uanzishwaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi kutoka Benki ya Biashara Tanzania (TCB) na kuitambulisha
Kamati ya Kitaifa ya kuratibu Hamasa na Elimu kwa Wanawake kujiunga na Majukwaa hayo.
Waziri Dkt. Gwajima amesema, lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Wananchi wanazifahamu fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi likiwemo kundi la Wanawake.
Akizungumzia kwenye hafla hiyo, Waziri Dkt. Gwajima amesema, jukumu la Kamati hiyo ya kitaifa ni kuratibu Wadau wengine wote kushiriki kwenye zoezi hili endelevu la kuhamasisha na kutoa elimu kwa wanawake walio kwenye majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi ili wafahamu faida za kujiunga kupitia Kampeni ya ‘Inuka-Imarika-Tusua Kiuchumi’.
“Natoa wito kwa Wadau wote wa maendeleo kushirikiana na Kamati hii niliyoitambulisha rasmi leo Aprili 8, 2025 ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa” amesema Dkt. Gwajima.
Ameongeza kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo imekuwa ikitekeleza jukumu la kuwawezesha Wanawake Kiuchumi ambapo, kutokana na uzoefu wa utekelezaji huo ilifanya mapitio ya Mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wa mwaka, 2022 na kutoa toleo la mwaka 2024 linaloendana na mahitaji ya sasa.


Comments
Post a Comment