MONGELLA: WANAWAKE TUMUWEKE SAMIA MADARAKANI KULINDA BEIJING

Na Bright DAR ES SALAAM: Mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati wa haki za wanawake, Gertrude Mongella, amewahimiza wanawake nchini kuhakikisha Rais Samia Suluhu Hassan anarudi madarakani katika uchaguzi ujao ili kuendeleza na kukamilisha mpango kazi wa kuwawezesha wanawake, unaotokana na maazimio ya Mkutano wa Beijing. Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mkutano wa Beijing, Mongella alisema wanawake wanapaswa kuona nafasi ya kuwa na Rais mwanamke kama agenda yao kuu.
“Ninajivunia sana. Juzi nilikuwa nje ya nchi, nikiona jinsi dunia inavyotazama mafanikio yetu. Sasa tunaye Rais mwanamke, tusipolinda hili kama ajenda yetu, ni bahati tunayoipoteza,” amesema Mongella kwa msisitizo. Aliongeza kuwa kurejea kwa Rais Samia si suala la kisiasa pekee, bali ni suala la kiuchungu kuhusu mwelekeo wa ajenda ya usawa wa kijinsia kama ilivyoainishwa katika Beijing Platform for Action.
“Naomba Samia arudi ili kuimarisha ajenda yetu kwamba mwanamke anaweza. Hili nalisema kwa uchungu wa Beijing, si kwa siasa,” ameeleza. Mongella alionya kuwa kutomchagua Rais Samia ni sawa na kuvunja heshima ya mafanikio ya mkutano wa Beijing. Aidha, alihimiza kuwepo kwa uwiano wa kijinsia katika nafasi za uongozi serikalini, akibainisha kuwa wanawake wana haki ya kumwajibisha Rais baada ya uchaguzi kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo.
Pamoja na hayo, Mongella aliitaka Tanzania kuachana na utegemezi wa misaada na badala yake kutumia rasilimali zilizopo kwa maendeleo, huku akihimiza wanawake kutumia elimu walizonazo kwa ubunifu na maendeleo. “Utafutwe mkakati wa kuwawezesha watoto wa kike kutengeneza na kutumia teknolojia. Elimu ya watu wazima irudishwe jioni — twende tukasome TEHAMA — maana dunia inaelekea huko,” alisema. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, aliwataka wanawake kupendana, kupeana fursa, na kusimamia maadili, hasa wakati huu wa mabadiliko ya kisasa. “Matunda ya Beijing ni ongezeko la wanawake katika nafasi za maamuzi. Wengi wao sasa wanafanya kazi kwenye sekta ya kilimo na nyingine, na hivyo wameleta mabadiliko chanya,” alisema. Alisisitiza umuhimu wa elimu kwa vijana, hasa waishio vijijini, na kuwataka wanawake kutimiza wajibu wao kwa kuhimiza amani wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu. Naye Profesa Penina Mlama kutoka taasisi ya Women Fund Tanzania-Trust alisema mkutano wa Beijing umeleta mageuzi makubwa kwa sababu ulilazimisha serikali nyingi kuingiza usawa wa kijinsia katika sera zao. “Tukumbuke mkutano huu ulikuwa muhimu sana. Tunampongeza mama Mongella kwa kuliongoza kwa umakini hadi kufanikisha tamko moja linalozingatia matakwa ya dunia nzima,” alisema Prof. Mlama.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA