DKT MWINYI: AMAN, UTULIVU NA ULIPAJI KODI, NGUZO ZA MAENDELEO ZANZIBAR
Amani, Utulivu na Ulipaji Kodi: Nguzo za Maendeleo Zanzibar Rais Dk. Mwinyi
Brigitter Zanzibar,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyopatikana visiwani humo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kudumu kwa amani, utulivu, mshikamano wa kitaifa na ulipaji mzuri wa kodi.
Akizungumza na jopo la wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, katika mkutano uliofanyika Ikulu ya Zanzibar baada ya kutembelea miradi mikubwa ya maendeleo Unguja na Pemba, Dk. Mwinyi amesema kuwa maendeleo ya Zanzibar yanaletwa na wananchi wenyewe kupitia ushirikiano wao na Serikali.
“Siri kubwa ya mafanikio haya ni upendo, mshikamano, na ushirikiano wa wananchi. Serikali imeweza kutekeleza miradi mikubwa kwa sababu ya mazingira ya amani na utulivu pamoja na ukusanyaji mzuri wa mapato,” amesema Rais Mwinyi.
Dk. Mwinyi amebainisha kuwa ukusanyaji mzuri wa kodi umeiwezesha Serikali kuendesha miradi ya kimkakati kwa kutumia fedha za ndani pamoja na mikopo kutoka taasisi za kimataifa, huku akisisitiza kuwa Zanzibar kwa sasa inaaminika zaidi na taasisi za kifedha duniani kutokana na utaratibu mzuri wa kulipa madeni.
“Zanzibar inakopesheka, kila mtu anataka kuikopesha. Hii ni kwa sababu tumeonyesha uwezo wa kusimamia madeni na miradi ya maendeleo kwa uwazi na ufanisi,” ameongeza.
Akiangazia hatua zinazofuata, Rais Mwinyi amesema kuwa Serikali katika awamu ijayo – endapo itapewa tena ridhaa na wananchi – itaweka mkazo katika kutatua changamoto zilizobaki katika sekta muhimu kama vile maji, afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Kuhusu sekta ya maji, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji katika mikoa ya Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Mjini Magharibi ambayo itamaliza kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi kwa wananchi wa maeneo hayo katika kipindi kifupi kijacho.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wahariri wakuu na waandishi wa habari waliopata fursa ya kuona mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu, huduma za jamii na uwekezaji katika sekta ya uchumi.
Mwisho



Comments
Post a Comment