JKCI YASHEREKEA MIAKA KUMI NA KUOKOA MABILIONI KATIKA MATIBABU YA MOYO

Na Brighitte DAR ES SALAAM:TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu kuanzishwa mwaka 2015 imeokoa maisha ya watu zaidi ya milioni moja na kuokoa fedha kiasi cha Sh bilioni 172 ambazo zilikuwa zinatumika kupeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi. Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka 10 ya utoaji wa huduma za matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi wa JKCI ,Dk Peter Kisenge amesema wanategemea kuokoa maisha ya watu wengi zaidi miaka ijayo hasa katika wakati huu ambao wanajikita katika matumizi ya akili mnembe. Dk Kisenge amesema katika miaka 10 wamefanya maendeleo makubwa hata hivyo bado wanaendelea kupanua huduma za moyo nchi kwa kujenga hospitali ya moyo ya watoto yenye vitanda 100 katika eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam.
"Kwa sasa JKCI siyo tu ni Hospitali ya Tanzania bali ya Africa kwani wagonjwa kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika kama India, Uturuki, China, Ufaransa, Ujerumani, wanatibiwa hapa, hivyo kuifanya JKCI kuikomboa Afrika kwenye masuala ya Moyo”, alisema Dkt. Kisenge Aidha amesema miongoni mwa mafanikio makubwa waliyopata ni kufanya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua teknolojia ambayo ni mpya zaidi duniani. "JKCI tumeweza kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimesaidia katika kuleta mafanikio ya taasisi, pia tumeajiri watumishi waliokuwa wanafanya kazi Hospitali ya Dar Group ambayo sasa ni tawi la JKCI", amesema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge amesema JKCI imetoa huduma za tiba mkoba kwa kuifikia mikoa 16 ya Tanzania na kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo wananchi ambao wengi wao wasingeweza kuzifuata huduma mahali zilipo. "Tunataka JKCI iwe India ya Afrika kwa kuwa kituo mahiri kwa matibabu ya moyo.zamani wagonjwa wengi walikuwa wanapelekwa South Africa lakini sasa wanaletwa hapa haya ni mafanikio makubwa kwetu,"ameeleza. Amesema JKCI tayari imeingia makubaliano na nchi mbalimbali za Afrika katika matibabu ya moyo na mafunzo kama vile nchi za Zambia,Burkina Faso ,Comoro na wagonjwa wa nje wanaendelea kuja kupata matibabu. Mwakilishi wa Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Ubungo , Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema taifa limeshuhudia kupungua kwa matumizi ya fedha za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa muda wa miaka 10 tangu mwaka 2015 wakati Serikali ilipoanzisha Taaisi hiyo kutoa huduma bingwa bobezi za moyo.
“Serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuwekeza vifaa tiba vya kisasa kurahisisha na kutoa matibabu kuendana na technolojia" amesema Msando Msando amewataka wataalamu wa afya kufanya tafiti ambazo zitatumia lugha rahisi na kuwafikia watu wa kawaida na wadau mbalimbali nchini. Maadhimisho ya miaka 10 ya JKCI imeambatana na Shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na upimaji wa mgonjwa ya moyo kwa Wanafunzi Mkoani Pwani,upimaji kwa askari polisi na wananchi. Na pia imeandaa midahalo ya afya iliyokutanisha wataalamu wa afya na wanafunzi wa elimu ya sekondari kujadili kuhusu utalii tiba na namna ambavyo matibabu ya moyo yanaenda kuleta utalii tiba nchini. Pia Wataalamu wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini waliweza kushiriki katika mdahalo wa kisayansi na kubadilishana ujuzi mwisho

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA