MBETO HAKUNA WA KUCHUKUWA USHINDI WA CCM ZANZIBAR 2025 -2030

Na Brigitter Zanzibar Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonyesha kujiamini kwa hali ya juu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, kikisema kuwa hakina mashaka na ushindi wake visiwani Zanzibar kwa kipindi cha 2025 hadi 2030, kwa mujibu wa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis. Akizungumza baada ya uzinduzi wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Mwenyekiti Mao Tse Tung, Unguja, Mbeto amesema hakuna kizuizi chochote kwa CCM kushinda kwa kishindo.
Mbeto ameleza kuwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Dk. Mwinyi ndiyo yanayotoa uhakika wa ushindi, akisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana Unguja na Pemba ni uthibitisho wa utekelezaji bora wa sera za CCM. “CCM haina sababu ya kushindwa uchaguzi huu. Kimetekeleza kwa vitendo sera zake kwa ufanisi na viwango stahiki,” amesema Mbeto. Aidha, ameeleza kuwa chama hicho kinaendelea kupata sapoti kubwa kutoka kwa wananchi, kutokana na imani waliyonayo juu ya utendaji wa serikali ya sasa. “Siri ya ushindi wa chama chochote makini cha siasa ni maandalizi ya kimkakati, kioganaizesheni na kujipanga. Tumejiandaa kisawasawa, sasa tuko tayari kwa ushindi wa kidemokrasia,” amesema kwa kujiamini. Mbeto pia alipongeza kazi iliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, akisema kuwa mafanikio katika sekta za elimu, miundombinu, ustawi wa jamii, biashara, utalii, na usafiri wa anga ni miongoni mwa mambo yatakayoipa CCM ushindi mkubwa. “CCM itashinda kwa asilimia 85 ya kura za urais, hivyo mgombea wetu Dk. Mwinyi atarejea tena madarakani kwa ridhaa ya wananchi,” ameeleza. Ameongeza kuwa mafanikio ya kimaendeleo yaliyopatikana yamewavutia siyo tu wananchi wa ndani, bali hata wageni kutoka nje wanaotembelea visiwa hivyo. Kwa mujibu wa Mbeto, ushindi wa CCM si jambo la kubahatisha bali ni matokeo ya kazi ya muda mrefu, uwajibikaji na uongozi thabiti unaoongozwa na Dk. Mwinyi. Mwisho

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA