UTORO WA MADAKTARI PEMBA WAPUNGUA BAADA YA KUJENGWA NYUMBA ZA KISASA
Na Brigitte
Pemba, Zanzibar
TATIZO la utoro miongoni mwa madaktari katika Kisiwa cha Pemba limepungua kwa kiwango kikubwa baada ya serikali kuwajengea makazi ya kisasa karibu na Hospitali ya Abdalla Mzee, iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumza na Habari Leo wakati wa ziara ya wahariri iliyoandaliwa na Kamati Maalum ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM Zanzibar, Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Hamis Suleiman Hamis, amesema uboreshaji wa mazingira ya kazi umeongeza ari na ufanisi kwa madaktari.
“Madaktari sasa wanafanya kazi kwa bidii kwa sababu hatuna haraka, wala hatuna tunakowahi makazi yapo hapa hapa hospitalini. Tunashukuru kwa kujengewa nyumba; tunaingia na nguo tu,” amesema Dkt. Hamis.
Ameeleza kuwa hali ya utoaji huduma imeimarika kwa kiasi kikubwa, huku akimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa mradi huo wa nyumba za madaktari.
“Madaktari tunaishi maisha mazuri na hali ya afya imeimarika. nyumba nzuri za kisasa na inasehemu ya mazoezi na mazingura rafiki. Hayo yote ni juhudi za Mheshimiwa Rais Mwinyi kwa mradi huu aliotupatia,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Dkt. Hamis, hospitali hiyo kwa sasa ina madaktari bingwa saba wa fani mbalimbali, madaktari wa kawaida 13, na wauguzi 72. Kila daktari ana uwezo wa kuwahudumia wastani wa wagonjwa 10 kwa siku.
Kwa upande wake, mkazi wa Uwereni, Rahima Mohammed Haji, ameeleza kuridhishwa na huduma za afya zinazotolewa kwa sasa, akisema kuwa uwepo wa madaktari waliopo karibu umeongeza kasi ya upatikanaji wa matibabu.
“Tunashukuru Rais Mwinyi kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutuletea maendeleo sisi wananchi wake,” amesema Rahima.




Comments
Post a Comment