KUSITISHWA KWA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA KAMATI YA OLIMPIKI TANZANIA (TOC)

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesitisha mchakato wa Uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambao ulipangwa ufanyike Oktoba 04, 2025 kutokana na kukataliwa kwa rufaa iliyowasilishwa na uongozi wa TOC kwa Waziri wa wizara hiyo dhidi ya maamuzi ya msajili wa Vyama vya Michezo. Imebainishwa uamuzi huo wa kusitisha mchakato wa uchaguzi huo umefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 27(2) cha Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa iliyofanyiwa marekebisho Na. 6 ya mwaka 1971, pamoja na kanuni za Usajili wa Vyama vya michezo za mwaka 1999 kanuni ya 11 (6) na (7) ambao ulifikishwa TOC kwa barua yenye Kumb. Na. BA.58/280/01/05 ya tarehe 30 Mei 2025 na barua yenye Kumb. Na. CBA.52/280/01/01 ya tarehe 03 Septemba 2025. Katika taarifa iliyotolewa leo Septemba 09, 2025 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Hassan Mabuye imesema Mheshimiwa Waziri wa Wizara hiyo ametoa maelekezo hayo kwa kuwa TOC ilitangaza uchaguzi kwa kutumia Katiba ambayo sio halali na kutoa maagizo ya kusimamishwa mara moja kwa mchakato wa Uchaguzi wa TOC uliotangazwa na pia kuanzishwa mara moja kwa mchakato mpya wa uchaguzi wa TOC kwa kutumia katiba yake iliyoidhinishwa Novemba 26, 2020 na inayotambuliwa na Baraza la Michezo la Taifa. Aidha Uongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania umeelekezwa kuzingatia na kutekeleza maelekezo ya Waziri mwenye dhamana huku wadau wote wa michezo nchini wameelekezwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na serikali ili kulinda maslahi mapana ya michezo ndani na nje ya nchi.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA