WANAFUNZI NI MUHIMU KUPATIWA ELIMU YA FEDHA
Elimu ya fedha yatajwa kuwa muhimu kwa wanafunzi kukabiliana na changamoto.
Na Brighitte
WADAU wa elimu na maendeleo ya vijana wameeleza umuhimu wa wanafunzi kujifunza elimu ya fedha na ujasiriamali ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea, kujikimu katika maisha ya shule na baada ya kuhitimu masomo yao.
Wakizungumza katika Bonanza maalum la kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika kutekeleza miradi ya kibiashara kupitia Mradi wa Mshilo Club unaotekelezwa na taasisi ya Her Initiative, wadau hao wamesisitiza kuwa elimu ya fedha kwa wanafunzi ni njia bora ya kukabiliana na changamoto ya ajira.
Mradi huo ulioanzishwa mwaka 2019, unalenga kuwawezesha wasichana kubaki shuleni kwa kuwapatia ujuzi wa elimu ya fedha, ujasiriamali na masoko, ili waweze kuwa na maarifa ya kujikimu katika maisha hata baada ya masomo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Her Initiative, Lydia Charles amesema kuwa ujuzi huo huwasaidia wanafunzi kuelewa namna ya kusimamia fedha, kupanga matumizi na kuanzisha biashara ndogondogo.
"Ujuzi huu unawawezesha wanafunzi kujipatia kipato hata wanapokosa ajira baada ya kuhitimu. Tunawafundisha masuala ya fedha, ujasiriamali na masoko ili wajitambue na waweze kujiamini," amesema Lydia.
Kwa mujibu wa Lydia, mradi huo unatekelezwa katika shule kadhaa za kata, zikiwemo:
Shule ya Sekondari King’ong’o wamejikita katika kilimo cha mbogamboga,
Kiluvya mradi wa kinyozi,Dar es Salaam Girls uzalishaji wa bidhaa za lishe kama pilipili, ubuyu na karanga,
Kisaranga utengenezaji wa sabuni za kufulia na kuoshea vyombo.
Hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 591 wamenufaika na mradi huo. Mauzo ya bidhaa wanazozalisha yamechangia kutatua changamoto mbalimbali shuleni, zikiwemo upatikanaji wa taulo za kike kwa wanafunzi.
Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, Afisa Tarafa wa Ubungo, Agnes Kyando amepongeza juhudi hizo na kuwasihi wadau wa maendeleo kushirikiana na serikali kuhakikisha miradi kama hiyo inaendelea kusaidia vijana nchini.
"Ujuzi wanaoupata unawasaidia wanafunzi kujitambua, kutumia ubunifu wao kutafuta fursa zilizopo katika jamii na kujiandaa kujitegemea baada ya shule," amesema Kyando.
Katika bonanza hilo, shule zilizofanya vizuri katika kutekeleza miradi yao zilipatiwa zawadi na tuzo. Shule ya Sekondari Kisaranga iliibuka mshindi na kujipatia tuzo pamoja na kiasi cha fedha cha shilingi Milion moja na laki mbili kwa mafanikio yao katika mradi wa sabuni.









Comments
Post a Comment