ALAFA APATA UFADHILI WA KUSOMEA UHANDISI WA NDEGE
Arafa apata ufadhili wa kusomea Uhandisi wa Ndege
ARAFA Mazige, msichana mwenye ndoto ya kuwa mhandisi wa injini za ndege, amepata ufadhili wa masomo kupitia taasisi ya UNI-AID AFRICA na atasoma Shahada ya Uhandisi wa Ndege Chuo Kikuu cha JAIN nchini India.
Msichana huyo kutoka Mvomero mkoani Morogoro alipata msukumo kutoka kwa baba yake, Hashimu Mazige, ambaye ni mbunifu wa teknolojia licha ya kutosomea rasmi.
Alishuhudia baba yake akifufua gari lililokuwa limeharibika kwa miaka mitatu, jambo lililomtia moyo kuamini kuwa kila kitu kinawezekana.
Akizungumzia mafanikio yake, Arafa anawahamasisha wanafunzi wenzake wa kike kujituma kwa kufanya vizuri darasani na kutumia mitandao ya kijamii kutafuta fursa za kielimu.
"Nitaendelea kujifunza zaidi ya yale yanayofundishwa darasani ili kuleta maendeleo ya kiteknolojia na kuwasaidia wengine kama mimi,"amesema.
Baba yake Hashim Mazige amesema kila mtoto anaweza kufanikisha ndoto yake ikiwa atapewa mazingira sahihi.
"Watoto wangu nimewajenga wawe na fikra pana na wasiwe na mipaka katika ndoto zao. Wazazi tunapaswa kuwapa nafasi watoto wetu kujifunza mambo mapya na kuwahamasisha kufuata ndoto zao.”amesema.
Meneja wa UNI-AID AFRICA, Aloyce Mkwizu, amesema Arafa ni mmoja wa wanafunzi 1,000 wanaopata msaada mwaka huu, huku akitoa shukrani kwa serikali kwa kuendelea kusaidia vijana katika masomo ya sayansi.
“Leo tunasherehekea mafanikio ya Arafa, ambaye ni wa kwanza kati ya wanafunzi 1,000 ambao tunatarajia kuwasaidia mwaka huu. Mwito wangu kwa serikali nj kuendelea kutusapoti, wasichana bado ni wengi wanahitaji msaada, pia, wasichana wanavyoenda kusoma nje, inapunguza mzigo kwa bodi ya mikopo,"amesema.
Katika kuhakikisha wanawafikia wasichana wengi wenye ndoto za kusoma nje, wamechapisha jarida maalum linaloitwa Hope na kueleza fursa mbalimbali katika vyuo mbalimbali vya nje ambavyo wanaweza kupata ufadhili wa kimasomo.
Mwisho


Comments
Post a Comment