AGNESTA KAIZA AAHIDI MIKOPO KWA WANAWAKE, VIJANA NA WALEMAVU SIKU 100 ZA KWANZA
Agnesta Kaiza Aahidi Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Walemavu Ndani ya Siku 100 za Kwanza
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Agnesta Kaiza, ameahidi kwamba ndani ya siku 100 za kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wa jimbo hilo wanapata mikopo ya asilimia 10 kama inavyotakiwa kisheria.
Kaiza alitoa ahadi hiyo wakati wa kufunga kampeni zake katika Jimbo la Segerea, akisisitiza kuwa fedha hizo ni haki ya makundi maalum na zitarudishwa kwao ili ziweze kujikwamua kiuchumi kupitia vikundi vya ujasiriamali.
“Fedha hizo ni haki yao. Nitahakikisha zinarudi kwa walengwa ili ziweze kuwasaidia kuanzisha na kukuza biashara zao,” amesema Kaiza.
Mbali na hilo, Kaiza aliahidi kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, akibainisha kuwa tatizo la maji Segerea litakuwa historia endapo atapewa ridhaa ya wananchi.
“Nitahakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Shida ya maji Segerea itaisha, tutahakikisha kila kaya inapata huduma hiyo muhimu,” ameongeza.
Kuhusu sekta ya afya, Kaiza amesema ataboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kina mama wanajifungua salama na wanapata huduma bora katika vituo vya afya na hospitali zilizopo jimboni humo.


Comments
Post a Comment