WiLDAF TANZANIA NA GIZ WAWANOA WAANDISHI KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MTANDAONI WAKATI WA UCHAGUZI

WiLDAF Tanzania na GIZ Waandaa Kambi Maalum ya Mafunzo kwa Waandishi wa Habari Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni na Wakati wa Uchaguzi
Brigitte Davis DAR ES SALAAM Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF Tanzania) kwa kushirikiana na GIZ limeendesha Kambi Maalum ya Mafunzo kwa Waandishi wa Habari kwa muda wa siku tatu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka 2025. Mafunzo hayo pia yanalenga kuunga mkono juhudi za kitaifa kupitia Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ukatili wa Kidijitali na Ukatili Dhidi ya Wanawake katika Uchaguzi.
Kambi hiyo imewaleta pamoja waandishi wa habari na wataalamu wa mawasiliano ili kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali ikiwemo uhusiano kwa umma, maadili ya mawasiliano, uandishi wa habari wenye weledi, usalama wa kidijitali, na usimulizi wa maudhui yanayozingatia usawa wa kijinsia na haki za binadamu. Kupitia mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kupata ujuzi wa namna bora ya kuripoti matukio yanayohusu ukatili wa kijinsia kwa uadilifu, weledi, na kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma, huku wakitumia teknolojia kwa usalama na manufaa ya kijamii.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya, alisema mpango huo ni sehemu ya jitihada endelevu za kujenga mtandao wa wanahabari wanaochochea mabadiliko ya kijamii kupitia uandishi unaolinda hadhi, haki na usawa wa kijinsia.
“Tunataka kuona waandishi wa habari wanakuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti za wanawake na wasichana, kupinga ukatili wa aina zote, na kutumia teknolojia kwa njia salama na chanya,” amesema Wakili Kulaya. Kwa upande wake, mwakilishi wa GIZ alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya habari katika kupambana na ukatili unaochochewa na teknolojia, hasa ule unaowalenga wanawake katika siasa na uchaguzi.
“Kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika bila hofu ni msingi wa demokrasia. Kupitia mafunzo haya, tunajenga kizazi cha waandishi wa habari wanaotetea haki, usawa na uwajibikaji wa kijamii,” ameongeza.
Kambi hiyo pia ni maandalizi ya Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Ukatili Unaotokana na Teknolojia na Ukatili Dhidi ya Wanawake katika Uchaguzi, ambapo wadau kutoka serikali, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wadau wa maendeleo wanatarajiwa kujadili mikakati ya pamoja ya kukomesha ukatili wa kijinsia mtandaoni na nje ya mtandao.
WiLDAF Tanzania na GIZ wamesisitiza dhamira yao ya kuendelea kuwekeza katika elimu, uhamasishaji na ubunifu wa kimawasiliano, ili kukuza jamii yenye usawa wa kijinsia na yenye heshima kwa haki za binadamu.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA