SERIKALI KUZALISHA NGUVU KAZI YENYE UJUZI, UBUNIFU KWA KUKUZA UCHUMI WA VIWANDA

Na Brigitter DAVIS DAR ES SALAAM:SERIKALI imepongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kuandaa mkutano muhimu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na kuongeza ujuzi wa nguvukazi nchini. Akizungumza katika mkutano huo kati ya VETA, wamiliki wa viwanda, waajiri na wadau wa ufundi stadi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, alisema Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), inayolenga kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi, ubunifu na tija katika soko la ajira. Amesema lengo ni kuhakikisha Tanzania inazalisha nguvukazi yenye ujuzi na umahiri unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira na maendeleo ya viwanda nchini. Profesa Nombo alisema Serikali kupitia VETA imeendelea kuboresha mitaala, miundombinu na mbinu za ufundishaji ili kuhakikisha mafunzo yanayolewa yanakidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma. Kwa sasa, kuna vyuo vya ufundi stadi zaidi ya 900 nchini, ambapo VETA inasimamia vyuo 80 vinavyotoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 300,000 kwa mwaka.
Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujenga vyuo vingine 64 katika wilaya mbalimbali na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe, hatua inayolenga kufikia vyuo 145 ifikapo mwaka 2026. “Hii itawezesha wananchi kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza tija katika shughuli za kijamii na kiuchumi,” amesema Profesa Nombo. Aidha, amesema VETA imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kutoa mafunzo ya vitendo, ubunifu na ujasiriamali. Ushirikiano huo umewezesha wanafunzi kupata mafunzo katika makampuni ya madini kama Barrick, Geita Gold Mining na North Mara, pamoja na mahoteli makubwa ya kitalii katika miji ya Arusha, Dar es Salaam, Tanga na Moshi. Kupitia programu ya Urasimishaji wa Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi (RPL), maelfu ya Watanzania wamefanikiwa kupata vyeti vya kitaalam na kutambulika rasmi, hatua iliyowawezesha kupata ajira na kuinua kipato chao. Akizungumzia miradi ya kimkakati, Profesa Nombo alisema VETA imeshiriki kikamilifu katika mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kutoa mafunzo maalum yaliyowawezesha Watanzania kushiriki katika ujenzi na usimamizi wa bomba hilo. Aliongeza kuwa hadi mwaka 2024, kulikuwa na zaidi ya viwanda 8,400 vilivyosajiliwa nchini, ikiwemo zaidi ya 200 vikubwa, vinavyotoa mchango mkubwa katika ajira na pato la Taifa. “Ukuaji wa viwanda unaibua mahitaji makubwa ya nguvukazi yenye ujuzi wa kisasa. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, zaidi ya ajira 700,000 mpya zitahitajika katika sekta za viwanda, nishati na ujenzi,” amesisitiza Profesa Nombo. Ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda na waajiri kufungua milango kwa vijana kupata mafunzo ya vitendo pamoja na kutoa nafasi kwa wakufunzi kupata uzoefu mpya kupitia programu za mafunzo viwandani. Aidha, amewataka wadau hao kushirikiana na VETA kuendeleza programu za Uanagenzi Rasmi (Dual Apprenticeship Training System – DATS) ambazo zimeonesha mafanikio makubwa katika kuandaa wahitimu wenye ujuzi mtambuka unaokidhi mahitaji ya soko la ajira. “Viwanda vina nafasi kubwa ya kusaidia ubunifu wa wanafunzi. Fanyeni makubaliano ya kibiashara kati ya VETA, wabunifu na viwanda ili bunifu ziwe bidhaa za kibiashara,” amesisitiza.
Akihitimisha hotuba yake, Profesa Nombo aliagiza VETA na wadau wa sekta hiyo kuendelea na utaratibu wa kukutana angalau mara moja kwa mwaka kujadili mafanikio, changamoto na mikakati mipya ya kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi na ubunifu wa hali ya juu itakayochochea maendeleo ya viwanda na ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasole, alisema awali walikuwa na vyuo 37 pekee lakini sasa vimeongezeka hadi 80 na wanatarajia kukabidhiwa vingine 60 vinavyoendelea kujengwa. Alisema VETA itaendelea kuhakikisha mafunzo bora yanatolewa kupitia mitaala bora, miundombinu imara na wakufunzi waliopata mafunzo ya kisasa. Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Msifuni Mchome, Makamu Mwenyekiti Clotilda Ndezi aliwataka wadau wa sekta ya viwanda na teknolojia kuendelea kutoa mafunzo kwa vitendo kulingana na mabadiliko ya mfumo wa kidijitali, ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la kisasa.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA