CRDB WAKUTANA NA MAWAKALA MIAMALA ZAIDI YA MILlONI 200 ZAPITIA KWA WAKALA

Miamala Zaidi ya Milioni 200 Yenye Thamani ya Trilioni 70 Zapitia Mawakala wa Benki ya CRDB Zaidi ya miamala milioni 200 yenye thamani ya takribani Shilingi trilioni 70 imefanyika kupitia mawakala wa Benki ya CRDB nchini kote katika kipindi cha mwaka mmoja. Kati ya kiasi hicho, zaidi ya Shilingi trilioni 3 ni makusanyo ya Serikali yaliyopokelewa kupitia mfumo wa uwakala wa benki hiyo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano na mawakala wa Benki ya CRDB, Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Muhinuliza Buberwa, amesema mafanikio hayo yanaonesha jinsi huduma za kifedha kupitia mawakala zinavyochangia kukuza ujumuishi wa kifedha na kuongeza mapato ya Serikali. Buberwa amesema kwa sasa Benki ya CRDB ina zaidi ya mawakala 45,000 nchini, sawa na asilimia 55 ya mawakala wote wa huduma za kifedha nchini.
“Kuwepo kwa idadi kubwa ya mawakala ni jitihada kubwa ya Benki ya CRDB, lakini mafanikio haya yasingepatikana bila ushirikiano wenu mawakala. Kwa sasa, sehemu kubwa ya miamala ya kifedha inapitia mfumo huu wa uwakala,” amesema Buberwa. Ameongeza kuwa, kumekuwa na mapinduzi makubwa katika kipindi cha miaka 12 tangu kuanzishwa kwa huduma za uwakala, hususan kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali na maboresho ya huduma.
Kwa mujibu wa Buberwa, kwa sasa hakuna tofauti kubwa kati ya mteja anayehudumiwa katika tawi la Benki ya CRDB na yule anayepata huduma kupitia wakala, kwani huduma zote muhimu zinapatikana kwa urahisi kupitia mfumo huo. Katika hatua nyingine, Buberwa amesema benki hiyo imezindua huduma bunifu ijulikanayo kama Tokenization, ambayo itawawezesha wateja wa CRDB — hata wale wasio na akaunti — kutoa fedha walizotumiwa kupitia wakala yeyote wa CRDB bila kutozwa gharama ya ziada. “Huduma hii inamwezesha mteja wa CRDB kutuma pesa kwa mtu yeyote, bila kujali kama ana akaunti au la. Mteja ataingia kwenye simu yake, kuchagua sehemu ya ‘tokeni’, kisha kuingiza namba ya simu ya mpokeaji. Mpokeaji atapokea ‘code’ ambayo ataenda nayo kwa wakala wa CRDB na atapatiwa fedha zake,” ameeleza Buberwa. Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawakala na Huduma za Malipo wa Benki ya CRDB, Catherine Lutenge, amesema semina hiyo imehusisha zaidi ya mawakala 800 kutoka Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia mawakala wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Mawakala walioshiriki katika semina hiyo wamesema wamepata elimu muhimu kuhusu matumizi sahihi ya mashine za POS, jambo ambalo wamelitaja kuwa litaboresha ufanisi katika utoaji wa huduma zao.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA