MSAMA WANANCHI WA DAR TUJITOKEZE KUMPOKEA RAIS SAMIA

Na Brighitte Dar es Salaam Aliyekuwa mtia nia wa Ubunge Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Production, Alex Msama, ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumpokea na kushiriki katika kampeni za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM na mgombea urais kupitia chama hicho. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Msama alisema ujio wa Rais Samia katika jiji hilo ni tukio muhimu linaloonesha dhamira yake ya kukutana na wananchi na kuwasikiliza moja kwa moja kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Amesema Rais Samia amekuwa akipokelewa kwa shangwe na hamasa kubwa katika mikoa yote aliyoitembelea, jambo linaloonyesha mapenzi makubwa ya wananchi kwake. “Rais wetu amezunguka katika mikoa mingi na kila alipofika amepokelewa kwa furaha kubwa. Sasa anakuja Dar es Salaam, hivyo ni jukumu letu wakazi wa jiji hili kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumuunga mkono katika kampeni zake ambazo zitafanyika katika maeneo ya Kinondoni, Ilala na Temeke,” amesema Msama. Aidha, Msama amewaasa wananchi wa dini zote na makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika kampeni hizo kwa amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda. “Nchi yetu ni nchi ya amani, kama ambavyo vyombo vya ulinzi vimeeleza kwamba uchaguzi utakuwa wa amani na utulivu. Tuwapuuze wale ndugu zetu wanaoishi mataifa ya mbali wanaotaka kutuvurugia amani. Sisi tunaishi Tanzania na tutaendelea kudumisha utulivu wetu,” ameongeza Msama.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA