VIJANA WAELIMISHWA UHIFADHI WA MAZINGIRA KUPITIA MRADI WA PLAY TO ZERO
Vijana waelimishwa kuhusu uhifadhi wa mazingira kupitia Mradi wa Play to Zero
Na Brigitter
Kisarawe
Wadau mbalimbali wa mazingira wamepanda miti 100 katika Shule ya Sekondari Minaki, Wilaya ya Kisarawe, kupitia Mradi wa Play to Zero, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Zoezi hilo limehusisha wanafunzi na walimu wa shule hiyo pamoja na washiriki wa mradi, ambapo walipanda miti kwa vitendo na kutoa elimu ya mazingira kwa wanafunzi. Lengo ni kuwajengea vijana uelewa wa umuhimu wa misitu katika kuhifadhi hewa safi, kupunguza joto duniani, na kukuza utamaduni wa utunzaji wa mazingira shuleni.
Mradi wa Play to Zero unatekelezwa kwa ushirikiano wa taasisi kadhaa zikiwemo Africa Carbon Agency, Klabu ya Mpira wa Miguu ya Africa Lyon, Swiss Tanzania Chamber of Commerce, na Hajakaa Ya Mwisho Foundation. Wadau hawa wamejipanga kukuza ushiriki wa vijana katika michezo na uhifadhi wa mazingira, wakiamini kuwa michezo inaweza kuwa njia bora ya kuhamasisha vitendo vya kulinda mazingira.
Mwakilishi wa Africa Carbon Agency, Magreth Lubusa, alisema kuwa upandaji miti ni hatua muhimu katika kulinda mazingira na mustakabali wa dunia. “Vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira yao. Mti mmoja unaopandwa leo ni uwekezaji katika maisha bora ya kesho,” amesema.
Baada ya shughuli ya upandaji miti, washiriki walipata fursa ya kutembelea Msitu wa Asili wa Pugu–Kazimzumbwi, ambapo walijionea vivutio vya kiasili na kujifunza kuhusu historia ya eneo hilo. Pia walishiriki chakula cha pamoja kama ishara ya mshikamano, ujirani mwema na dhamira ya pamoja ya kulinda mazingira.
Kampeni hiyo inaungwa mkono na mamlaka mbalimbali za uhifadhi ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), na inalenga kuibua kizazi cha vijana kinachotenda kwa vitendo katika kupanda na kutunza miti kama sehemu ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.




Comments
Post a Comment