KARIKAKOO YAZINDUA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Kariakoo Yazindua Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, Yatangaza Msamaha wa Kodi kwa Wafanyabiashara Walioathirika na Moto Na Brigitter Davis SHIRIKA la Masoko la Kariakoo limezindua rasmi Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2025 kwa dhamira ya dhati ya kuwasaidia wafanyabiashara, ambapo limetangaza msamaha wa kodi ya pango kwa miezi miwili kwa wamiliki wa maduka yaliyoharibiwa na moto uliowahi kutokea.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Ashiraf Abdulkarim, Meneja Mkuu wa Mipango wa Shirika la Masoko la Kariakoo, alisema wiki hii imelenga kuboresha huduma na kujenga upya imani kwa wafanyabiashara kwa kuhakikisha wanarejea katika biashara kwa usalama na utulivu. “Tumetoa msamaha wa kodi ya miezi miwili kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao kwenye moto. Wiki hii pia inalenga kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa haraka,” amesema Abdulkarim.
Ameongeza kuwa maandalizi ya kuwapatia wafanyabiashara maeneo mapya ya biashara yamekamilika, na biashara zilizoathirika zimeruhusiwa kuanza ujenzi upya wakati huu wa msamaha wa kodi. Kwa lengo la kuboresha mazingira ya soko, Abdulkarim alieleza kuwa nafasi zaidi ya 400 za maegesho zimeandaliwa ili kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za biashara.
Kwa upande wake, Omary Yusuf Yenga, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Dar es Salaam, alisema uzinduzi wa soko jipya la Kariakoo ni mwanzo wa mapinduzi ya kibiashara ndani na nje ya Tanzania. “Biashara haiwezi kustawi bila soko la kisasa. Tunashukuru kwa kuwa na soko lenye miundombinu imara na usalama wa uhakika. Hili litachochea ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema Yenga. Amesifu pia juhudi za kuwawezesha wafanyabiashara kupitia semina za uongozi, akisema mafunzo hayo yataongeza ufanisi na tija kazini.
Severine Mushi, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kariakoo, ametangaza kuwa ofisi rasmi za viongozi sasa zitakuwa ndani ya soko hilo, hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji na kuboresha huduma kwa wateja. “Tunataka kukuza uchumi wa taifa kupitia soko hili. Kutokana na changamoto zilizopita, tunapendekeza malipo ya kodi yaanze tena Januari ili kuwapa wafanyabiashara muda wa kujiimarisha,” ameongeza Mushi.
Steven Lusinde, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wadogo (Wamachinga), aliahidi ushirikiano wa karibu na Shirika la Masoko Kariakoo ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora. Katika kumalizia, Happy Njovu, Meneja wa Soko la Kisutu, aliipongeza menejimenti ya Kariakoo kwa juhudi zao za kuboresha mazingira ya biashara. “Tunashukuru kwa soko hili zuri na la kuvutia. Wiki ya Huduma kwa Wateja inaonesha dhamira ya kweli ya Kariakoo katika kuboresha biashara na maisha ya wafanyabiashara wake,” amesema Njovu.

Comments

Popular posts from this blog

MATAIFA 8 KUIMBA TAMASHA LA PASAKA

PIMEA USIKU WA WANA NDOA ULIVYOFANA MSIFICHANE NA KUWEKEANA VITU

UONGOZI DHAIFU VYATAJWA KUVURUGA TAASISI ZA VIJANA