ASILIMIA 39.5 YA WANAWAKE WAATHIRIKA WA UKATILI; SERIKALI YATAHADHARISHA HATARI YA UKATILI WA KIDIJITALI
DAR ES SALAAM: Serikali imesema ukatili wa kijinsia unaendelea kuwa moja ya changamoto kubwa za haki za binadamu nchini, huku takwimu za kitaifa zikionesha kuwa asilimia 39.5 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamewahi kukumbwa na ukatili wa aina mbalimbali, ikiwemo wa kimwili, kihisia na kingono kutoka kwa wenza wao.
Aidha, wadau wameitaka jamii kuimarisha usalama wa kidijitali na kushughulikia ukatili wa kijinsia unaowezeshwa na teknolojia (TFGBV), ili kuruhusu wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika elimu, fursa za kiuchumi, uongozi na maisha ya kiraia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kitaifa kuhusu viashiria vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika kupitia teknolojia (TFGBV), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Abeda Rashid Abdallah, amesema kuwa tatizo hilo linaongezeka kwa kasi na linahitaji hatua za haraka.
Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la C-Sema, ukiwa na lengo la kuimarisha juhudi za Tanzania katika kukabiliana na ongezeko la ukatili wa kidijitali dhidi ya wanawake na watoto.
Akifafanua zaidi, Abeda amesema ukatili huo unaojumuisha vitendo kama usambazaji wa picha za faragha bila ridhaa, unyanyasaji wa kingono mtandaoni, vitisho vya kidijitali pamoja na lugha za chuki na matusi, unaathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa kisaikolojia na kijamii wa waathirika, hususan wanawake na wasichana.
Amesema zaidi ya nusu ya wanawake vijana wamewahi kukumbana na unyanyasaji mtandaoni, hali inayozua wasiwasi mkubwa hasa katika kipindi hiki ambacho matumizi ya teknolojia yanaongezeka kwa kasi nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini Tanzania, Melissa Barrett, amesema teknolojia inapaswa kuwa chombo cha kuwawezesha watu badala ya kuwa jukwaa la kuumiza.
“Ni muhimu ubunifu wa kidijitali uchangie katika kukuza usawa wa kijinsia na kulinda haki za binadamu,” amesema Barrett.
Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting, amesema kupitia ushirikiano kati ya serikali ya Finland, UNFPA na Serikali ya Tanzania, wanashirikiana kuboresha usalama wa mtandao, utawala wa kidijitali na matumizi ya teknolojia yenye kuzingatia maadili.
Amesema juhudi hizo zinalenga kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanasaidia kupunguza ukatili wa kijinsia badala ya kuongeza pengo hilo.
Kwa upande wake, Ofisa Programu za Jinsia kutoka UNFPA, Ally Ahmad, amesema mkutano huo una umuhimu mkubwa katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu changamoto ya ukatili wa kijinsia unaochochewa na matumizi ya teknolojia nchini.
Amesema kupitia majadiliano ya wadau mbalimbali wakiwemo serikali, taasisi za kimataifa, wataalamu wa teknolojia na wanajamii, mikakati madhubuti itaandaliwa ili kukabiliana na tatizo hilo kwa ufanisi zaidi.





Comments
Post a Comment